Skip to content
-
Subscribe to our newsletter & never miss our best posts. Subscribe Now!
Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

  • Home
  • Sample Page
  • Home
  • Sample Page
Close

Search

  • https://www.facebook.com/
  • https://twitter.com/
  • https://t.me/
  • https://www.instagram.com/
  • https://youtube.com/
Subscribe
Habari

Serikali yasitisha leseni ya MwanaHALISI, TEF yapinga

By admin
August 19, 2026 4 Min Read
Comments Off on Serikali yasitisha leseni ya MwanaHALISI, TEF yapinga

Dar es Salaam. Serikali imesitisha leseni ya gazeti la MwanaHALISI kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Agosti 19, 2026 kwa kile ilichoeleza, limekiuka masharti kwa kuchapisha maudhui yaliyokosa usahihi, mizania na uthibitisho wa kutosha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari Maelezo, uamuzi huo umefikiwa kutokana na habari iliyochapishwa katika toleo namba 571 la Agosti 6 hadi 12, 2026, lenye kichwa cha habari ‘Nchimbi agoma kujiuzulu’.

Hata hivyo, adhabu hiyo imepingwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), lililosema halikubaliani na uamuzi huo kwa kuwa, umetolewa na chombo ambacho chenyewe ndicho kinachoshitaki na kinachohukumu.


Hiyo ni adhabu ya pili inayohusisha usitishwaji wa leseni kwa vyombo vya habari tangu kuanza kwa mwaka 2026. Aprili 2, mwaka huu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ilisitisha leseni ya utangazaji ya Jambo Online TV kwa siku 90.

Jambo Online iliadhibiwa kwa kosa la kurusha maudhui yaliyodaiwa kupotosha umma kuhusu hali ya matukio, Machi 31, 2026.

Adhabu kama hiyo, iliikumba Asasi ya Kiraia ya JamiiForums, iliyositishiwa leseni yake ya huduma za maudhui mtandaoni na TCRA kwa siku 90, kuanzia Septemba 6, mwaka jana na adhabu yake iliisha mapema mwaka huu.

Taarifa ya Maelezo kuhusu kusitishwa kwa leseni hiyo, imetolewa leo, Jumatano Agosti 19, 2026 ikirejea kifungu cha 9(b) cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, baada ya kujiridhisha kuwa gazeti hilo limeendelea kurudia makosa ya kitaaluma licha ya kupewa maonyo ya awali.

Taarifa hiyo, imeeleza kabla ya kufikiwa kwa uamuzi huo, Mkurugenzi wa Huduma za Habari aliipa MwanaHALISI fursa ya kusikilizwa katika kikao kilichofanyika Agosti 7, 2026 katika ofisi za Maelezo jijini Dar es Salaam.

Baada ya kikao hicho, gazeti hilo lilipewa siku tatu kuwasilisha maelezo ya maandishi ili kufafanua mazingira yaliyopelekea kuchapishwa kwa habari husika. Hata hivyo, maelezo yaliyowasilishwa hayakutosha kuondoa hoja zilizowasilishwa dhidi ya gazeti husika.

“Miongoni mwa dosari zilizobainishwa katika habari iliyosababisha adhabu hiyo ni matumizi ya picha ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, huku maelezo yaliyokuwa chini ya picha hiyo yakimtaja Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Maelezo, hali hiyo ilionyesha upungufu katika mchakato wa uhakiki na uhariri wa habari kabla ya kuchapishwa.

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa habari husika ilikosa mizania kwa kuwa ilijadili mada ya madai ya kujiuzulu kwa Dk Nchimbi bila kuonyesha mahali popote ambapo mhusika huyo alihojiwa au kutoa kauli yake kuhusu suala hilo.

Aidha, ilidaiwa kuwa gazeti lilinukuu hoja zinazodaiwa kutolewa na Makonda bila kuwasilisha uthibitisho unaoonyesha kuwa alitamka kauli hizo.

“Mwandishi wa habari hiyo hakuwahoji viongozi wa Chama cMapinduzi (CCM) wala washiriki wa kikao kilichodaiwa kujadili suala hilo ili kuthibitisha madai yaliyokuwa yamewasilishwa kupitia vyanzo vya habari visivyotajwa wazi,” imeeleza taarifa hiyo.

Mbali na dosari hizo, Maelezo imeeleza ilizingatia pia historia ya gazeti hilo ya kupewa maonyo katika matukio yaliyopita.

Miongoni mwa matukio hayo ni lile la Februari 2026 baada ya kuchapishwa kwa habari yenye kichwa ‘Samia wa 2021 atakutana lini na wa 2026?’, ambayo kwa mujibu wa Maelezo ilimwelezea Rais Samia Suluhu Hassan kwa lugha isiyozingatia misingi ya taaluma ya habari. Kufuatia tukio hilo, wahariri wa gazeti hilo waliitwa katika kikao na kupewa onyo la mdomo.

Aidha, Mei mwaka huu gazeti hilo lilitakiwa kujieleza kuhusu maudhui yaliyokuwa katika toleo namba 557 lenye vichwa vya habari ‘ICC haikwepeki’, ‘Hawa kuchongewa’ na ‘Watang’oka tu’.

Baada ya maelezo na utetezi wake kusikilizwa, Maelezo ilitoa onyo la maandishi na kuwataka wahariri wake kuimarisha umakini katika uhakiki wa maudhui na usahihi wa taarifa kabla ya uchapishaji.

“Kwa kuwa dosari zilizobainika katika habari ya hivi karibuni zilifanana na zile zilizokuwa zimeonywa hapo awali, Maelezo imeona kuna msingi wa kutoa adhabu kali zaidi,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Maelezo, kusitishwa kwa leseni hiyo kunahusisha pia usambazaji wa gazeti hilo kwa njia za kielektroniki na mtandaoni katika kipindi chote cha adhabu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Huduma za Habari, gazeti la MwanaHALISI lina haki ya kukata rufaa kwa waziri mwenye dhamana ya habari ndani ya siku 30 tangu tarehe ya kutolewa kwa uamuzi huo.

Katika taarifa hiyo, Maelezo pia ilibainisha kuwa MwanaHALISI limekuwa likikiuka Kanuni ya 6(1) ya Kanuni za Huduma za Habari inayovitaka vyombo vya habari kuwasilisha nakala za machapisho yao kwa Mkurugenzi wa Huduma za Habari kila yanapotolewa.

Idara hiyo imewataka wamiliki wote wa vyombo vya habari nchini kuzingatia matakwa ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na kuonya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kuendelea kukiuka sheria hiyo.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema mara zote na kwa njia yoyote hakubaliani na uamuzi wa usitishaji wa leseni za vyombo vya habari.

“Chombo kinachotoa leseni, kiwe na mamlaka yanayojitegemea, kisiwe chenyewe ndio mlalamikaji na mtoa hukumu,” amesema.

Amesisitiza hawezi kukubaliana na utaratibu wa ufungiaji leseni kwa vyombo vya habari, ama viwe vimefanya kosa au vinginevyo.

Amesema kama kuna mtu aliyetendewa kosa kutokana na maudhui katika chombo cha habari, njia sahihi ni kufuata vyombo vya kisheria kwa maana mahakama ili hukumu iendane na mizania ya Katiba na sheria nyinginezo.

Aidha, Balile, amesema kwa upande wa wanahabari wanapaswa kutambua kuwa, kila haki ina wajibu na wanapoandika habari ni vema wazingatie msingi wa ukweli.

“Ukiulizwa hili suala likoje uwe na uwezekano wa kuthibitisha. Hizi kauli za kwenye korido tusiziandike maana siku utaitwa kwenye vyombo vya sheria ukashindwa kujitetea. Sasa tuangalie kama tunafanya sawa kwa mujibu wa misingi ya taaluma au tunakosea tukisubiri kutetewa,” amesema Balile.

Jamvi la Habari nao waitwa

Katika hatua nyingine, Maelezo imesema imeliandikia gazeti la Jamvi la Habari kulitaka lifike katika kikao na kuwasilisha maelezo kuhusu baadhi ya maudhui yaliyochapishwa katika matoleo ya Agosti 15 na Agosti 17, 2026, ambayo idara hiyo inaamini yanaweza kuwa yamekiuka masharti ya Sheria ya Huduma za Habari na kanuni zake.

Author

admin

Follow Me
Other Articles
Previous

Kilomita sita kufuata matibabu zawasukuma Kola kujenga zahanati 

Next

Sh4.9 bilioni zalipwa kwa waliopisha mradi wa maji Chamwino Ikulu

Recent Posts

  • DC HAI AENDELEA KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI, ATATUA MIGOGORO YA ARDHI
  • Wamiliki miundombinu muhimu ya Tehama watakiwa kuisajili
  • SHILINGI BILIONI 356 ZATUMIKA KUTEKELEZA MIRADI MOROGORO
  • Binti auawa kwa madai ya kupigwa na baba yake mdogo, kisa sherehe ya tohara
  • PROF. MKUMBO: HALMASHAURI ZIBUNI SHUGHULI MPYA ZA KIUCHUMI, SI TOZO MPYA.

Recent Comments

  1. A WordPress Commenter on Hello world!

Archives

  • August 2026

Categories

  • Habari
  • Magazeti
  • Michezo
Copyright 2026 — Habarimpya. All rights reserved. Blogsy WordPress Theme