Kilomita sita kufuata matibabu zawasukuma Kola kujenga zahanati
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kusisitiza umuhimu wa kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, wakazi wa Kijiji cha Kola, Wilaya ya Kisarawe, wamejichangisha fedha na kujitolea nguvu kazi kujenga zahanati baada ya kukabiliwa na changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata matibabu.
Wananchi hao wamesema hulazimika kutembea kati ya kilomita tano na sita kufuata huduma za afya katika vijiji vya Kisanga na Kifuru, hali inayowaathiri zaidi wajawazito, watoto na wazee.
Changamoto hiyo inajitokeza licha ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015–2020 kuahidi kujenga zahanati katika kila kijiji na kuzipatia vifaa tiba, kwa lengo la kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, kupunguza adha ya kutembea umbali mrefu na kudhibiti vifo vinavyoweza kuepukika.
Hata hivyo, wakazi wa Kola wamesema bado hawajapata zahanati katika eneo lao, hali iliyowasukuma kuchukua hatua wenyewe kwa kujichangisha fedha na kujitolea nguvu kazi kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Kwa makubaliano yao, kila mkazi mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea anatakiwa kuchangia Sh4,500. Hadi sasa, wamekusanya Sh600,000 ikiwa ni mwanzo wa utekelezaji wa mradi huo.
Wananchi wa Kijiji cha Kola wakiwa kwenye kikao cha ujenzi wa Zahanati ya Kijiji kilichofanyika Augosti 17, 2026. Picha na Jumanne Bakana.
Aidha, wananchi hao wametenga eneo lenye ukubwa wa hekta 12 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo.
Hata hivyo, kiasi hicho bado ni kidogo ikilinganishwa na gharama za ujenzi wa zahanati, ambazo kwa mujibu wa viwango vya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), zinakadiriwa kuwa kati ya Sh284 milioni na Sh358 milioni, kutegemea eneo na gharama za ujenzi.
Juhudi hizo za wananchi zinafanyika wakati Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikiweka msisitizo katika kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, hususan maeneo ya vijijini, kwa kuimarisha miundombinu ya afya ya msingi na kupunguza umbali na muda unaotumika kufuata matibabu.
Akizungumza katika kikao cha maendeleo ya mradi huo kilichofanyika Agosti 17, 2026, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, Mjumbe na Msaidizi wa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kola, Joseph Malima, amesema wananchi wamechukua hatua hiyo baada ya kuona umuhimu wa kuwa na huduma za afya karibu na makazi yao.
“Tumekuwa tukitembea umbali mrefu kupata matibabu. Sasa tumeamua kujitolea fedha na nguvu kazi ili wananchi wetu wapate huduma karibu na makazi yao,” amesema Malima.
Amesema changamoto hiyo huwa kubwa zaidi wakati wa msimu wa masika kutokana na ubovu wa barabara na uwepo wa misitu katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Malima, maandalizi ya ujenzi wa zahanati hiyo yalianza Julai 25, 2025, baada ya wananchi kukutana na kutenga eneo kwa ajili ya mradi huo.
Jitihada hizo zimepokelewa na uongozi wa Wilaya ya Kisarawe, ambao umeahidi kushirikiana na wananchi kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Nyahori Nyang’ari, amechangia malori mawili ya kokoto kwa ajili ya kuanza ujenzi wa msingi wa zahanati hiyo.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Kata ya Kola, Beatrice Kiula, amesema wananchi wako tayari kushirikiana na Serikali kukamilisha ujenzi huo.
“Wananchi wapo tayari kuungana na Mkuu wa Wilaya kusudi kutimiza lengo letu la kuwa na zahanati hapa, na tunaomba Serikali iendelee kutuunga mkono,” amesema Kiula.
Wananchi wa Kijiji cha Kola wakiwa kwenye kikao cha ujenzi wa Zahanati ya Kijiji kilichofanyika Augosti 17, 2026. Picha na Jumanne Bakana.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Dk Grayson Mramba, amesema Idara ya Afya ipo tayari kupeleka vifaa tiba na wataalamu mara tu zahanati hiyo itakapokamilika.
“Kituo cha afya kipo mbali sana. Wananchi hulazimika kwenda Kisanga au Kazimzumbwi, kwa hiyo maeneo haya yanahitaji huduma za afya.
“Nawapongeza wananchi kwa kujitolea kwenu. Sisi kama Idara ya Afya tupo pamoja nanyi na tutahakikisha zahanati inapokamilika, vifaa tiba pamoja na wataalamu vinapelekwa kwa haraka,” amesema Dk Mramba.
Ujenzi wa zahanati hiyo unatarajiwa kuanza Agosti 24, 2026, huku Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Magoti, akiwa amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika hatua ya kwanza ya ujenzi.
Magoti amewataka wanaume, wanawake na vijana kujitolea katika ujenzi huo, huku akiahidi kuratibu msaada wa kilo 50 za mchele kutoka kwa wawekezaji wa eneo hilo kwa ajili ya chakula cha wananchi watakaoshiriki.
“Vijana mjitokeze kwa wingi. Kina mama ambao mnajitolea kuchota maji, tutaweka utaratibu wa kupata chakula hapa. Kola kuna wawekezaji wengi, tutamuomba mmoja wao awasaidie na kuwaletea kilo 50 za mchele,” amesema Magoti.
Ujenzi huo unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika juhudi za wananchi wa Kola kusogeza huduma za afya karibu na makazi yao, huku Serikali ikiendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha mradi huo unakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

