Skip to content
-
Subscribe to our newsletter & never miss our best posts. Subscribe Now!
Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

  • Home
  • Sample Page
  • Home
  • Sample Page
Close

Search

  • https://www.facebook.com/
  • https://twitter.com/
  • https://t.me/
  • https://www.instagram.com/
  • https://youtube.com/
Subscribe
Habari

Ebola yazidi kutikisa DR Congo, vifo vyafikia 2,378

By admin
August 19, 2026 3 Min Read
Comments Off on Ebola yazidi kutikisa DR Congo, vifo vyafikia 2,378

Dar es Salaam. Mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umefikia kiwango cha kutisha, huku idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa ikifikia 5,021 na vifo 2,378 tangu ulipotangazwa Mei mwaka huu.

Takwimu hizo zilizotolewa na mamlaka za afya nchini humo hadi jana, Agosti 18, zinaonyesha ukubwa wa mlipuko huo unaoendelea kuenea katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mlipuko huo unasababishwa na aina ya virusi vya Ebola vya Bundibugyo, na sasa ni miongoni mwa milipuko mikubwa zaidi kuwahi kurekodiwa.



Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Ghebreyesus, amesema kasi ya maambukizi ni kubwa ikilinganishwa na milipuko mingine ya Ebola iliyowahi kutokea.

Amesema hali hiyo imechangiwa na ukosefu wa usalama katika baadhi ya maeneo, uhamaji wa watu pamoja na ongezeko la safari kupitia barabara na mito, ikiwamo harakati za wafanyakazi katika maeneo ya uchimbaji madini.

“Mlipuko huu bado haupo karibu kudhibitiwa,” amesema Tedros.

Amesema changamoto nyingine ni kuwa maambukizi yalikuwa tayari yamesambaa katika jamii kabla ya mlipuko huo kutambuliwa rasmi, hali iliyoongeza ugumu wa kuyadhibiti.

WHO imesema kinachotia wasiwasi zaidi ni idadi ya wagonjwa wanaofariki wakiwa majumbani au katika jamii bila kufikishwa kwenye vituo vya afya.

Hali hiyo, kwa mujibu wa WHO, inaweza kufanya baadhi ya wagonjwa kutotambuliwa na hivyo kuongeza uwezekano wa virusi kuendelea kuenea kwa watu wanaowazunguka.

Taarifa ya WHO inaonyesha mlipuko huo umeenea katika majimbo sita ya DRC na kufikia maeneo 55 yanayosimamiwa na mfumo wa afya, huku Ituri ikiwa miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi.

Thierno Balde, anayesimamia mwitikio wa WHO dhidi ya mlipuko huo, amesema bado kuna uwezekano wa kuudhibiti ndani ya miezi mitatu ikiwa rasilimali zinazohitajika zitapatikana.

Balde amesema WHO inahitaji takribani dola 115 milioni (takribani Sh302.5 bilioni) kwa ajili ya shughuli za kukabiliana na mlipuko huo, lakini hadi sasa imefanikiwa kupata karibu asilimia 60 ya fedha hizo.

Katika kukabiliana na hali hiyo, WHO imeongeza vitanda vya matibabu na wataalamu wa kufuatilia watu waliokutana na wagonjwa, huku ikishirikiana na mamlaka za afya za Congo kuimarisha uchunguzi, ufuatiliaji na matibabu.

Hata hivyo, juhudi hizo zinakabiliwa na changamoto za upungufu wa miundombinu ya afya, migogoro katika baadhi ya maeneo na harakati kubwa za watu.

Wafanyakazi wa migodi ya dhahabu wanaohama kutoka eneo moja kwenda jingine wametajwa kuwa miongoni mwa makundi yanayoongeza changamoto katika kufuatilia mienendo ya maambukizi.

WHO pia imesema aina ya Bundibugyo inayosababisha mlipuko huo haina chanjo wala tiba maalumu iliyoidhinishwa kwa sasa, ingawa tafiti na majaribio ya chanjo na tiba zinaendelea.

Kutokana na hali hiyo, WHO imesisitiza umuhimu wa kugundua wagonjwa mapema, kuwafuatilia watu waliokutana nao, kuimarisha vituo vya afya na kushirikisha jamii katika hatua za kuzuia maambukizi.

Kwa upande mwingine, Umoja wa Mataifa (UN) umeonya kuwa mwitikio wa afya dhidi ya mlipuko huo unakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na kasi ya maambukizi.

UN imetaka kuongezwa kwa haraka kwa rasilimali na msaada kwa mamlaka za Congo ili kuzuia mlipuko huo kuenea zaidi.

Author

admin

Follow Me
Other Articles
Previous

ATOLEWA JIWE LA KILO 3.1 KWENYE KIBOFU

Next

MAONESHO YA YST YAIBUA HAMASA YA SAYANSI KWA WANAFUNZI LINDI

Recent Posts

  • Kilomita sita kufuata matibabu zawasukuma Kola kujenga zahanati 
  • FIFA IMEJIHARIBIA YENYEWE KWA MPANGO WA KOMBE LA DUNIA – MKUU WA LIGI KUU YA UINGEREZA
  • SERIKALI YATOA MIEZI SITA KUSAJILI MIUNDOMBINU MUHIMU YA TEHAMA
  • MAONESHO YA YST YAIBUA HAMASA YA SAYANSI KWA WANAFUNZI LINDI
  • Ebola yazidi kutikisa DR Congo, vifo vyafikia 2,378

Recent Comments

  1. A WordPress Commenter on Hello world!

Archives

  • August 2026

Categories

  • Habari
  • Magazeti
  • Michezo
Copyright 2026 — Habarimpya. All rights reserved. Blogsy WordPress Theme