Skip to content
-
Subscribe to our newsletter & never miss our best posts. Subscribe Now!
Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

  • Home
  • Sample Page
  • Home
  • Sample Page
Close

Search

  • https://www.facebook.com/
  • https://twitter.com/
  • https://t.me/
  • https://www.instagram.com/
  • https://youtube.com/
Subscribe
Habari

NIKWAMBIE MAMA: Mkulima na mfugaji ni gego na ufizi, havitengani

By admin
August 19, 2026 4 Min Read
Comments Off on NIKWAMBIE MAMA: Mkulima na mfugaji ni gego na ufizi, havitengani

Kwenye simulizi moja nilipata kusikia kisa kinachonifikirisha hadi leo. Kisa kilichonikumbusha kuwa sukari na chumvi vyote ni muhimu kwa mwanadamu, japo haviwezi kuwekwa kwenye chombo kimoja. Mtu atakunywa chai na muhogo wa kuchemsha, ataweka sukari kwa chai na chumvi kwa kitafunwa. Akibadilisha viungo au kuchanganya vyote kwa pamoja, staftahi haitakamilika na mlo hautalika.



Nilihadithiwa kisa cha mama mmoja mjane kutoka Mikoa wa Kaskazini. Aliolewa na mwanaume wa huko na kubarikiwa watoto wawili. Baada ya miaka miwili ya upweke, alikutana na mwanaume wa kutoka Pwani. Akaolewa tena na kuhamia kwa mumewe. Mume alitimiza majukumu yake kama baba, lakini mama hakuzoea utamaduni wa Pwani. Alipofanya kosa la kizembe alipewa pole, akaombwa kwa upole kutolirudia.

Alianza kummisi mume wake wa kwanza, ambaye angemrarua hadi ngozi kwa kosa la kuunguza mboga. Pia alianza kuchukia maisha ya huku Pwani kwani alipomtwanga mwanawe, majirani na Serikali ya Mtaa waliingilia kuamua ugomvi. Alikumbuka kule kwao ambako ndugu na majirani walimsaidia mtu aliyetembeza kichapo. Kwa mtindo huu ndoa yake haikudumu, alirudi kwao kuishi maisha aliyokwisha kuyazoea.

Malezi yanalemaza sana. Ukitaka kumtesa mtoto wa uswahilini, mpe ratiba ya kila siku wakati wa likizo yake. Aamke saa moja, aoge na kunywa maziwa saa mbili. Saa tatu aende twisheni, saa nane arudi, aoge, kula na kulala. Saa kumi ajisomee mpaka saa mbili usiku. Ale na kulala tena! Jumamosi na Jumapili badala ya twisheni, ajifunze kupitia vipindi vya Watoto TV na kuunga ratiba ya kila siku.

Wenyewe wameshazoea kurudi nyumbani ni mpaka asikie kelele za mama. Mama atapiga kelele hizo pale anapohitaji kumtuma mtoto sokoni. Uswahilini mama habembelezi mtoto kula, anasema “mwache tu, akisikia njaa atarudi mwenyewe”. Na mtoto wa Mbagala akishazoea hivyo, ukimpeleka Masaki kwenye nyama, kuku, maziwa na mayai atakonda. Kupangiana ratiba si maisha yake. Atatoroka, maana kuku wa kienyeji halishwi bandani.

Pale mwanzoni hali ilikuwa mbaya sana. Watu wa makabila tofauti hawakuweza kuishi pamoja kutokana na tofauti ya tamaduni zao. Kabila lilipigana na kabila katika kulinda mipaka na utamaduni wake. Haikuwezekana kwa Mmasai kuishi au kuoa Mzaramo kwani malezi yao yalikuwa tofauti sana. Mmoja alikuzwa akikamua ng’ombe, na mwingine alikuwa akikesha mkoleni akiwa mgongoni mwa mamaye.

Mambo yalianza kubadilika baada ya uhuru. Asilimia kubwa ya Watanzania walipelekwa shule hata kama hawakutaka. Watu wakachanganya tamaduni japo si kwa hiyari; mtumishi wa Serikali kutoka Bara alihamishwa na familia yake kuja Pwani, mwingine wa Bagamoyo alipelekwa kuwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Babati. Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Temeke alipelekwa Shule ya Upili Tabora, na kadhalika.

Wakaanza kuzoeana na hatimaye kuoana na kujenga familia. Hivi sasa tofauti za tamaduni zimezidi kupungua. Vizazi vinachangia udugu wa “baba wa Kaskazini mama wa Kusini”. Au baba mwenye wake watatu anakutanisha tamaduni za makabila manne kwenye familia moja. Wote wanauishi utamaduni wa Kitanzania: Kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi wanashiriki shughuli za maendeleo kwa pamoja.

Lakini pamoja na hatua tuliyofika, ni lazima tukubali kuwa kuna mushkeli mkubwa ndani ya jamii yetu. Sababu kubwa ya tofauti zao zinatokana na maeneo ya kuishi na kufanyia pilika zao. Kumekuwa na misuguano ya muda mrefu baina ya wakulima na wafugaji. Hawa wote ni walewale wanaotegemea maeneo yenye rutuba, yanayoweza kuzalisha chakula cha binadamu na mifugo.

Wazo langu kuu litaigusa Serikali moja kwa moja. Tanzania ni nchi yenye maeneo makubwa yasiyotumika. Kama vile inavyotenga maeneo ya uchimbaji madini, uvuvi, viwanda na michezo, vivyo hivyo itayarishe maeneo kwa ajili ya ufugaji. Izingatiwe kuwa watu na mifugo wanaongezeka, lakini ardhi inabaki kuwa vilevile. Iundwe sera ya kutayarisha maeneo mapya kwa ajili ya malisho ya wanyama, yatakayosaidia miaka mingi ijayo.

Jambo la pili: Serikali inapowahamisha wakazi wa eneo fulani kupisha uwekezaji, iwe tayari imeshatayarisha mustakabali wa wahamaji. Haitoshi kuwalipa fidia pekee, watengewe maeneo ambayo watafanya shughuli zao bila kuzuiwa au kuingiliwa kwa namna yoyote.

Hii itaepusha wafugaji kuingilia maeneo ya wakulima, au kuingiliwa na wakulima. Visingizio vya wafugaji “kupitisha mifugo mashambani” vitakoma.

La tatu: Wakulima na wafugaji waanze kuunganishwa kwenye mambo yanayowakutanisha. Kilimo na ufugaji ni sekta zinazobebana. Bila samadi mmea usingemea, na bila mimea wanyama wasingeishi. Sekta hizi mbili zina udugu wa kuku na yai, bila kimoja kingine kisingalikuwapo. Ndio maana masomo yake huwekwa pamoja, na kwenye nchi nyingi sekta hizi zimekuwa zikiunganishwa katika Wizara moja.

Hivyo wangepewa elimu ya kuishi pamoja ingekuwa poa zaidi. Ni vipi tuliweza kuyaunganisha makabila zaidi ya mia na watu zaidi ya milioni 60, tushindwe kutuliza sekta hizi mbili? Tuliweka historia ya kupata uhuru bila kuuana, na tukatatua matatizo yetu wenyewe bila kuzogomana.

Kama mawazo ya zamani yanafeli basi ipo haja kubwa ya kuitisha midahalo na kukaribisha mawazo mapya. Tanzania ni yetu sote.

Author

admin

Follow Me
Other Articles
Previous

UCHAMBUZI WA MAYALA: Elimu, ujuzi, ubunifu ndiyo msingi wa maendeleo

Next

Upinzani na safari ya ujenzi wa kizazi kipya chenye ushawishi

Recent Posts

  • Usaliti wa ACT – Wazalendo, Chadema katika sura pana
  • Serikali yaeleza kusuasua mradi wa Hospitali ya Singida – 3
  • FYATU MFYATUZI: Naunda tume tatu kuchunguza tume
  • Upinzani na safari ya ujenzi wa kizazi kipya chenye ushawishi
  • NIKWAMBIE MAMA: Mkulima na mfugaji ni gego na ufizi, havitengani

Recent Comments

  1. A WordPress Commenter on Hello world!

Archives

  • August 2026

Categories

  • Habari
  • Magazeti
  • Michezo
Copyright 2026 — Habarimpya. All rights reserved. Blogsy WordPress Theme