Skip to content
-
Subscribe to our newsletter & never miss our best posts. Subscribe Now!
Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

  • Home
  • Sample Page
  • Home
  • Sample Page
Close

Search

  • https://www.facebook.com/
  • https://twitter.com/
  • https://t.me/
  • https://www.instagram.com/
  • https://youtube.com/
Subscribe
Habari

Serikali yaeleza kusuasua mradi wa Hospitali ya Singida – 3

By admin
August 19, 2026 5 Min Read
Comments Off on Serikali yaeleza kusuasua mradi wa Hospitali ya Singida – 3

Dar es Salaam. Kuchelewa kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida ni sehemu ya mlolongo mpana wa changamoto katika usimamizi wa fedha, mikataba na utoaji wa huduma za afya, imebainika.



Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa, licha ya mradi huo kuanza mwaka wa fedha 2016/17, bado haujakamilika, hivyo kuibua maswali kuhusu usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya afya na uzingatiaji wa matakwa ya Kanuni ya 242(2) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2013.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe, anasema kanuni inaelekeza mkandarasi anapochelewesha mradi anatakiwa kulipa fidia kwa kuchelewa, kwa kuzingatia masharti maalumu ya mkataba.

Vivyo hivyo, mwajiri anawajibika kulipa fidia iwapo atashindwa kutekeleza wajibu wake na madai hayo yakathibitishwa kitaalamu.

Kanuni hiyo inasisitiza usimamizi madhubuti wa mikataba ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati, ndani ya gharama zilizokubaliwa na kwa kuzingatia viwango vya ubora vilivyokusudiwa.

Kwa mujibu wa kanuni hiyo, taasisi za umma zinatakiwa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mikataba ili changamoto zibainike mapema na hatua stahiki zichukuliwe kabla hazijasababisha ucheleweshaji mkubwa.

Imebainika katika uchunguzi kuwa mradi huo umepitia mabadiliko ya wakandarasi, kusitishwa kwa mikataba, maboresho ya usanifu na ucheleweshaji wa utekelezaji.

Kwa mujibu wa nyaraka za Serikali, mradi huo uliingizwa kwenye mipango ya maendeleo katika mwaka wa fedha 2016/17, huku mchakato wa zabuni ukianza mwaka uliofuata.

Lengo lilikuwa kuimarisha na kukamilisha hospitali hiyo ifikapo Juni 2019, lakini mpaka sasa jengo kuu la ghorofa tatu bado linaendelea kujengwa.

Dk Magembe anasema mfumo wa kisheria unaweka wajibu kwa pande zote za mkataba kuhakikisha utekelezaji wa miradi unafanyika kwa wakati na kwa kuzingatia masharti yaliyokubaliwa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, kusuasua kwa mradi huo hakukutokana na ukosefu wa uwajibikaji, bali changamoto za utekelezaji zilizojitokeza katika awamu ya pili.

Dk Magembe anasema mkandarasi wa awamu ya pili, MCB–Chuo cha Mbeya, hakufanya kazi kwa kiwango kilichotarajiwa, jambo lililosababisha mkataba kusitishwa kwa makubaliano ya pande zote.

Anasema kutokana na namna mkataba ulivyositishwa, Serikali haikutoza fidia dhidi ya mkandarasi huyo.

“Baada ya hapo, wizara ilianza upya mchakato wa kumpata mkandarasi mwingine, hatua iliyohusisha maandalizi ya nyaraka za zabuni pamoja na kufanya maboresho ya usanifu wa mradi,” anasema Dk Magembe.

Anasema maboresho yalijumuisha kuongeza wodi za watu mashuhuri (VIP na VVIP), wodi za mifupa na kupanua kazi za nje ya jengo. Jambo hilo, anaeleza, lilimlazimu Chuo cha Ardhi, kama mshauri elekezi, kufanya upya michoro na BOQ kabla ya kuanza kwa awamu ya tatu.

Mradi huo kwa sasa unaendelea kutekelezwa na Hainan Co. Ltd, mkandarasi wa daraja la kwanza, chini ya usimamizi wa Chuo cha Ardhi.

Dk Magembe anasema wizara inafuatilia utekelezaji wa mradi huo kupitia mshauri elekezi kwa mujibu wa masharti ya mkataba.

Anasema hakuna mianya ya kisheria inayochelewesha utekelezaji wa miradi ya afya kwa sababu mikataba yote hupitiwa na wataalamu wa sheria kabla ya kusainiwa.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2021/22 inaonesha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida ilikuwa miongoni mwa miradi iliyobainika kuchelewa kukamilika, licha ya kuongezewa muda wa utekelezaji.

CAG anabainisha katika ripoti kuwa mradi huo, uliokuwa chini ya mkandarasi Anudha Limited, haukukamilika hata baada ya muda wa nyongeza wa mkataba kumalizika Agosti 12, 2022, hali iliyochelewesha upatikanaji wa huduma zilizotarajiwa kutokana na uwekezaji huo.

Ripoti ya CAG inaeleza ucheleweshaji huo ulihusisha mkataba wenye thamani ya Sh425.03 milioni, akieleza kuwa kutokamilika kwa mradi kwa wakati kunaweza kuathiri ufanisi wa matumizi ya fedha za umma na kuchelewesha wananchi kupata huduma za afya zilizolengwa.

Katika mahojiano na Mwananchi, Agosti 2026, CAG Charles Kichere anasema jukumu la ofisi yake si kubainisha upungufu pekee, bali pia kutathmini iwapo matumizi ya fedha za umma yameleta matokeo yaliyokusudiwa na kuwafikia wananchi.

Anasema ripoti ya mwaka wa fedha 2024/25 imebainisha changamoto kadhaa katika utekelezaji wa miradi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, ikiwamo ujenzi wa majengo matatu uliokuwa ukiendelea wakati wa ukaguzi. Majengo hayo ni wodi ya watoto, jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na wodi ya wagonjwa wa mifupa.

Kichere anasema ujenzi wa majengo manne ulikuwa haujaanza, ambayo ni karakana ya vifaa tiba na mitambo, karakana ya Tehama, eneo la huduma ya chakula, kituo cha kufulia nguo na jiko.

Anasema ujenzi wa kituo cha kudhibiti ugonjwa wa Uviko-19 haukukamilika kwa wakati, licha ya fedha kuwekwa katika Akaunti ya Amana Hazina Ndogo tangu Oktoba 2021.

Kichere anasema mkandarasi wa awali, Mbeya University, alishindwa kukamilisha kazi kwa mujibu wa mkataba.

Anasema baada ya tathmini na kusitishwa kwa mkataba huo, kazi zilikabidhiwa kwa China Hainan International na utekelezaji kwa sasa unaendelea.

“Dosari kuu zilizobainika ni ukosefu wa fedha kutoka Wizara ya Afya, kutotosheleza kwa makusanyo ya ndani kugharimia ujenzi, udhaifu katika usimamizi wa mkataba, kuchelewa kukamilika kwa miradi na kushindwa kutekeleza mpango wa ununuzi,” anasema na kuongeza:

“Hali hiyo ilisababisha utoaji hafifu wa huduma, msongamano wa wagonjwa, uhaba wa vitanda, rufaa za wagonjwa kwenda hospitali nyingine na gharama kubwa za kusafirisha oksijeni kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na Hospitali ya Benjamin Mkapa.”

Hata hivyo, anasema hakupima wala kuainisha kiwango cha ukiukwaji wa Kanuni ya 242(2) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2013.

“Kwa mwaka wa fedha 2024/25, shughuli za ununuzi zilisimamiwa chini ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na kanuni zake za mwaka 2024, badala ya sheria ya mwaka 2011 na kanuni za mwaka 2013 zilizorekebishwa mwaka 2016,” anasema.

Kichere anabainisha udhaifu katika usimamizi wa mkataba na kuchelewa kukamilika kwa kazi, huku hatua iliyochukuliwa ikiwa ni kusitisha mkataba wa Mbeya University na kukabidhi kazi kwa China Hainan International.

Anasema mkandarasi huyo yupo eneo la mradi na mkataba wake unatarajiwa kukamilika mwaka wa fedha 2026/27.

Kichere anashauri uongozi wa hospitali kufanya ufuatiliaji wa karibu na Wizara ya Afya ili fedha zinazohitajika zitolewe kwa wakati, ili kuwezesha mradi kukamilika.

Anasema ucheleweshaji wa mradi umezuia hospitali kupata kwa wakati manufaa yaliyokusudiwa, licha ya fedha na rasilimali kutengwa kwa ajili ya utekelezaji wake.

Anataja athari zilizobainika kuwa ni kuendelea kwa utoaji wa huduma katika kiwango kisichokidhi mahitaji kutokana na uhaba wa majengo, vitanda na vifaa.

“Msongamano wa wagonjwa katika maeneo machache yaliyopo, wagonjwa kuendelea kupelekwa katika hospitali nyingine, ikiwamo Bugando, KCMC na Hospitali ya Benjamin Mkapa, na hii imesababisha kuongezeka kwa gharama za rufaa na usafirishaji wa wagonjwa,” anasema.

Kutotekelezwa kwa mpango wa ununuzi, anasema, umesababisha wananchi kuchelewa kupata huduma za kibingwa karibu na maeneo yao.

“Kwa hiyo, ucheleweshaji huo unapunguza ufanisi, tija na uchumi katika matumizi ya fedha za umma na unaathiri moja kwa moja ubora na upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi,” anasema Kichere.

Author

admin

Follow Me
Other Articles
Previous

FYATU MFYATUZI: Naunda tume tatu kuchunguza tume

Next

Usaliti wa ACT – Wazalendo, Chadema katika sura pana

Recent Posts

  • Usaliti wa ACT – Wazalendo, Chadema katika sura pana
  • Serikali yaeleza kusuasua mradi wa Hospitali ya Singida – 3
  • FYATU MFYATUZI: Naunda tume tatu kuchunguza tume
  • Upinzani na safari ya ujenzi wa kizazi kipya chenye ushawishi
  • NIKWAMBIE MAMA: Mkulima na mfugaji ni gego na ufizi, havitengani

Recent Comments

  1. A WordPress Commenter on Hello world!

Archives

  • August 2026

Categories

  • Habari
  • Magazeti
  • Michezo
Copyright 2026 — Habarimpya. All rights reserved. Blogsy WordPress Theme