Skip to content
-
Subscribe to our newsletter & never miss our best posts. Subscribe Now!
Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

  • Home
  • Sample Page
  • Home
  • Sample Page
Close

Search

  • https://www.facebook.com/
  • https://twitter.com/
  • https://t.me/
  • https://www.instagram.com/
  • https://youtube.com/
Subscribe
Habari

Usaliti wa ACT – Wazalendo, Chadema katika sura pana

By admin
August 19, 2026 7 Min Read
Comments Off on Usaliti wa ACT – Wazalendo, Chadema katika sura pana

Agosti 12 kila mwaka, Umoja wa Mataifa huadhimisha Siku ya Vijana Duniani. Mwaka huu, siku hiyo ilitoa picha nyingine katika siasa za Tanzania baada ya jumuiya za vijana za Chadema na ACT-Wazalendo kutumia fursa hiyo kuonyesha nguvu na uhai wa taasisi zao.



Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) lilifanya kongamano Dodoma, huku Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo ikikutana Dar es Salaam. Kwa yeyote aliyekuwa na mashaka kuhusu uhai wa vyama hivyo, matukio hayo yalikuwa ishara kwamba vinaendelea kujenga kizazi cha vijana kinachoweza kuwa msingi wa siasa zao za sasa na baadaye.

Vijana ni uhai wa leo, lakini pia ni ahadi ya kesho. Chama cha siasa chenye vijana wengi wanaojengewa uwezo wa kiuongozi, kinajiwekea mazingira ya kuendelea kuwa na nguvu kisiasa kwa muda mrefu. Kadiri chama kinavyoongeza ushiriki wa vijana, ndivyo kinavyoimarisha nguzo zake za uhai na afya ya kisiasa.

Kwa mantiki hiyo, taasisi ya kisiasa isiyowekeza kwa vijana inaweza kukabiliwa na changamoto ya kizazi na hatimaye kupoteza ushawishi wake.

Historia ya vyama vya siasa inaonyesha umuhimu huo. Oktoba 2, 1920, kiongozi wa zamani wa Urusi na Umoja wa Kisovieti (USSR), Vladimir Lenin, alipohutubia Jumuiya ya Vijana ya Kikomunisti ya Urusi, alisisitiza umuhimu wa kujifunza kama msingi wa majukumu ya vijana.

Kwa mujibu wa falsafa hiyo, jumuiya za vijana zilipaswa kuwa sehemu ya kuwaandaa vijana kupitia elimu ya itikadi na uongozi ili waweze kuwa viongozi wa baadaye.

Afrika Kusini pia ina historia inayofanana. Mwaka 1944, Ashley Peter Mda, Walter Sisulu na Oliver Tambo waliposhiriki kuanzisha Jumuiya ya Vijana ya African National Congress (ANC Youth League), walilenga kujenga kizazi kipya cha viongozi wenye uwezo wa kuendeleza mapambano ya kisiasa dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Lengo halikuwa tu kuwaunganisha vijana, bali pia kuwajenga kuwa viongozi wenye busara, uzalendo na uwezo wa kuendeleza harakati za chama.

Mfano mwingine unatoka Namibia, ambako Jumuiya ya Vijana ya Swapo (Swapo Youth League) imekuwa na jukumu la kuwaandaa vijana katika misingi ya itikadi na uongozi wa chama hicho.

Tanzania nayo ina historia yake. Jumuiya ya Vijana ya Tanu, na baadaye Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), ililenga kuwajenga vijana kiitikadi, kiuongozi na kizalendo.

Hivyo, jumuiya za vijana hazipaswi kutazamwa kama sehemu za kuandaa mikutano au kampeni pekee. Zinapaswa kuwa shule za uongozi, fikra na uwajibikaji kwa vijana ambao baadaye wanaweza kushika nafasi mbalimbali ndani ya vyama na taifa.

Ndiyo maana kongamano la vijana wa Chadema na mkutano wa vijana wa ACT-Wazalendo una umuhimu zaidi ya matukio ya siku moja. Vinatoa picha ya namna vyama hivyo vinavyotengeneza kizazi kitakachobeba siasa zao katika miaka ijayo.

Katika kongamano la Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu, aliwataka vijana kutokuwa na hofu wala kuhadaika wanapokiita chama chao cha wasaliti, akisema wanaowaita hivyo ndiyo waasisi wa usaliti.

Ingawa hakukitaja moja kwa moja chama alichokuwa akikilenga, maudhui ya hotuba yake yalielekea kwenye mjadala wa uhusiano kati ya ACT-Wazalendo na Chadema, hasa kwa kuzungumzia historia ya tofauti za kisiasa kati ya vyama vya upinzani.

Kwa upande mwingine, ujumbe wa Jussa unaweza kutafsiriwa kama jitihada za kuwajenga vijana wa ACT-Wazalendo kujiamini na kujivunia taasisi yao. Katika siasa zenye ushindani mkali, tuhuma za usaliti zinaweza kuwafanya wanachama, hasa vijana, kuanza kuhoji uhalali wa msimamo wa chama chao.

Hata hivyo, katika siasa za vyama vingi, neno “usaliti” linahitaji kutumiwa kwa tahadhari. Vyama vya siasa vina katiba, itikadi, sera, falsafa na vipaumbele tofauti. Hivyo, kutofautiana kwa msimamo hakumaanishi moja kwa moja kwamba upande mmoja umemsaliti mwingine.

ACT-Wazalendo, kwa mfano, kilianzishwa mwaka 2014 na kupata usajili wa kudumu mwaka 2015. Baadhi ya waasisi wake walikuwa na historia ya kisiasa ndani ya Chadema. Uamuzi wao wa kuanzisha chama kingine ulikuwa sehemu ya mabadiliko katika siasa za upinzani nchini.

Katika mfumo wa vyama vingi, kila chama kinatafuta kupata uungwaji mkono wa wananchi na hatimaye kushinda uchaguzi. Kwa hiyo, Chadema na ACT-Wazalendo vinaweza kushirikiana katika jambo fulani, lakini wakati huo huo vikawa washindani katika uchaguzi au katika sera fulani.

Hali hiyo ni ya kawaida katika siasa. Vyama vinaweza kuungana pale vinapoona ushirikiano utawasaidia kufikia malengo fulani, lakini muungano huo hauondoi tofauti zao za msingi wala ushindani wa kisiasa.

Ndiyo maana ni sahihi zaidi kutumia maneno kama “kutofautiana mtazamo au msimamo” kuliko kukimbilia neno “usaliti” kila kunapotokea tofauti.

Kama chama kimoja kingekuwa kinakubaliana na kila uamuzi wa chama kingine, bila kujali itikadi, sera au maslahi yake, hoja ya uwepo wa ushindani wa vyama vingi ingepoteza maana.

Jambo la msingi ni kwamba ushindani wa kisiasa usigeuke kuwa uadui unaowagawa wananchi. Vyama vinaweza kutofautiana, kukosoana na kushindana, lakini vinaweza pia kushirikiana pale maslahi ya taifa yanapohitaji kufanya hivyo.

Zaidi ya yote, vijana wanaopikwa leo ndiyo watakaobeba vyama hivi kesho. Hivyo, Chadema, ACT-Wazalendo na vyama vingine vina wajibu wa kuhakikisha jumuiya zao za vijana zinakuwa shule za uongozi, uzalendo, maarifa na siasa zinazoheshimu tofauti za kimtazamo.

Kwa sababu chama kinaweza kuwa na sera nzuri, viongozi wenye uzoefu na historia ndefu, lakini bila kizazi kipya cha vijana wa kuendeleza taasisi hiyo, uhai wake wa kisiasa unaweza kudhoofika.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 1995, ambao ulikuwa wa kwanza kufanyika chini ya mfumo wa vyama vingi, Chama cha Wananchi (CUF) kiliongoza Kambi ya Upinzani Bungeni. Hata hivyo, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, CUF iligomea matokeo ya uchaguzi Zanzibar, hali iliyosababisha wabunge wake kutoka Unguja na Pemba kususia vikao vya Bunge.

Katika kipindi hicho, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiliongoza Kambi ya Upinzani Bungeni, huku aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Aman Walid Kabourou, akiwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni.

Baada ya kufikiwa kwa mwafaka Zanzibar na wabunge wa CUF kurejea bungeni, chama hicho kilipata idadi kubwa ya wabunge upande wa upinzani na kuunda Kambi ya Upinzani Bungeni. Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Wilfred Lwakatare, alichaguliwa kuwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni, huku Kabourou na timu yake ya Baraza la Mawaziri Kivuli wakiondolewa.

Matukio hayo yanaonyesha kwamba nafasi ya kuongoza upinzani haikuwa jambo la kudumu kwa chama fulani, bali ilitegemea mazingira na uwiano wa nguvu ndani ya Bunge.

Katika Bunge la Tisa, lililodumu kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, ushirikiano wa vyama vya upinzani ulikuwa mkubwa zaidi. CUF, ikiwa chama cha upinzani kilichokuwa na wabunge wengi, kilishirikiana na Chadema pamoja na UDP, iliyokuwa na mbunge mmoja.

Wakati huo, aliyekuwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed, alifanya kazi kwa karibu na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa. Ushirikiano wao ulionekana kama mfano wa namna vyama vya upinzani vinavyoweza kuweka tofauti zao pembeni na kufanya kazi kwa masilahi ya pamoja.

Hata hivyo, mazingira yalibadilika baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, ambapo Chadema kilipata wabunge wengi zaidi. Hatua hiyo ilibadili uwiano wa nguvu ndani ya upinzani.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, vyama vya upinzani viliunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), uliokuwa na lengo la kushirikiana katika uchaguzi na kupunguza mgawanyiko wa kura za upinzani. Freeman Mbowe, aliyekuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, aliwaunganisha wabunge wa CUF na NCCR-Mageuzi katika Baraza la Mawaziri Kivuli. Hata hivyo, baadaye aliwaondoa na kambi hiyo kubaki ikiendeshwa na Chadema.

Hapa ndipo tunapopaswa kujiuliza: Je, CUF ilipowahi kuwaondoa Chadema katika Kambi ya Upinzani Bungeni, ilikuwa inafanya usaliti?

Kama chama kinaona masilahi yake yanahitaji kufanya uamuzi fulani, hakiwezi kuitwa msaliti kwa sababu tu chama kingine hakikubaliani nacho. Vivyo hivyo, Chadema ilipoamua kuunda Kambi ya Upinzani Bungeni bila CUF au vyama vingine, haikuwa sahihi kuiita hatua hiyo usaliti. Ilikuwa ni sehemu ya siasa za ushindani na maamuzi ya chama.

Tatizo linapoanza ni pale neno “usaliti” linapotumiwa kuelezea kila tofauti ya kimtazamo au uamuzi ambao chama kimoja hakikubaliani nao.

Mfano mwingine ni suala la ACT-Wazalendo kuketi na CCM na kufikia makubaliano ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, kama inavyotakiwa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010. Hatua hiyo haiwezi kuitwa usaliti kwa sababu tu chama kingine hakikubaliani nayo.

Kwa upande wa Zanzibar, ushirikiano wa kisiasa una maana ya kipekee kwa sababu mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa umewekwa katika Katiba. Kwa hiyo, chama kinaposhiriki katika mchakato huo kinapaswa kupimwa kwa misingi ya masilahi ya wananchi na sheria, si kwa tofauti za kisiasa pekee.

Tukirudi mwaka 2015, CUF ilipinga uchaguzi wa Zanzibar na kususia uchaguzi wa marudio. Chadema, kwa upande wake, kilikataa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo kwa kauli, lakini kikaendelea na shughuli za Bunge na kuunda Kambi ya Upinzani Bungeni.

Je, kwa sababu hiyo Chadema ilikuwa imeisaliti CUF? Hapana. Kilifanya uamuzi wake kwa kuzingatia masilahi na mikakati yake ya kisiasa.

Kwa hiyo, neno “usaliti” linafaa kutumika kwa tahadhari. Ikiwa kuna mfano unaoweza kuingia katika tafsiri hiyo, ni pale vyama vinapofikia makubaliano ya wazi halafu mmoja wao akayavunja kwa makusudi.

Mfano unaweza kuwa katika mgawanyo wa majimbo wakati wa Ukawa mwaka 2015. Endapo makubaliano yalikuwa yamempitisha mgombea wa chama kimoja katika jimbo fulani, lakini chama kingine kikabaki na mgombea wake licha ya makubaliano, hatua hiyo ingeweza kuonekana kama kuvunja makubaliano.

Kwa mfano, katika Jimbo la Segerea, Julius Mtatiro wa CUF alitajwa kuwa mgombea wa Ukawa, lakini Anatropia Theonest wa Chadema aliendelea kuwepo kama mgombea wa chama hicho. Mgawanyiko huo wa wagombea ulisababisha kura za upinzani kugawanyika na Bona Kamoli wa CCM kushinda.

Huo ni mfano unaoweza kujadiliwa kama kuvunjwa kwa makubaliano kwa sababu kulikuwa na uamuzi wa pamoja uliokuwa umefikiwa.

Lakini tofauti za sera, misimamo au maamuzi ya ndani ya chama si lazima ziitwe usaliti. Kila chama kina vikao vyake, katiba yake, itikadi yake na masilahi yake ya kisiasa.

Vyama vya upinzani vinapaswa kuheshimiana hata vinaposhindana. Chadema hakiwezi kuwa shabiki wa ACT-Wazalendo, kama ambavyo ACT-Wazalendo hakiwezi kuwa shabiki wa Chadema kila wakati. Kila chama kinataka kushinda na kujenga ushawishi wake.

Kama chama kimoja kinakifurahia kingine, mara nyingi ni kwa sababu kuna jambo linalogusa masilahi yao kwa wakati huo.

Huo ndio uhalisia wa siasa za ushindani. Kinachopaswa kupewa uzito si kulazimisha vyama kuwa marafiki, bali kuhakikisha ushindani wao unafanyika kwa kuheshimu sheria, makubaliano, taasisi na masilahi mapana ya wananchi.

Author

admin

Follow Me
Other Articles
Previous

Serikali yaeleza kusuasua mradi wa Hospitali ya Singida – 3

Recent Posts

  • Usaliti wa ACT – Wazalendo, Chadema katika sura pana
  • Serikali yaeleza kusuasua mradi wa Hospitali ya Singida – 3
  • FYATU MFYATUZI: Naunda tume tatu kuchunguza tume
  • Upinzani na safari ya ujenzi wa kizazi kipya chenye ushawishi
  • NIKWAMBIE MAMA: Mkulima na mfugaji ni gego na ufizi, havitengani

Recent Comments

  1. A WordPress Commenter on Hello world!

Archives

  • August 2026

Categories

  • Habari
  • Magazeti
  • Michezo
Copyright 2026 — Habarimpya. All rights reserved. Blogsy WordPress Theme