Skip to content
-
Subscribe to our newsletter & never miss our best posts. Subscribe Now!
Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

  • Home
  • Sample Page
  • Home
  • Sample Page
Close

Search

  • https://www.facebook.com/
  • https://twitter.com/
  • https://t.me/
  • https://www.instagram.com/
  • https://youtube.com/
Subscribe
Habari

UCHAMBUZI WA MAYALA: Elimu, ujuzi, ubunifu ndiyo msingi wa maendeleo

By admin
August 19, 2026 4 Min Read
Comments Off on UCHAMBUZI WA MAYALA: Elimu, ujuzi, ubunifu ndiyo msingi wa maendeleo

Si mara moja wala mbili nimekuwa nikisema na kuandika kwamba Tanzania si nchi maskini. Tatizo letu kubwa ni umasikini wa kupanga na kuweka vipaumbele, unaotokana na kushindwa kutumia kikamilifu rasilimali na fursa tulizonazo.



Tanzania imejaaliwa rasilimali nyingi, ikiwamo ardhi yenye rutuba, vyanzo vya maji, madini ya aina mbalimbali, maliasili za utalii na nafasi nzuri ya kijiografia. Imezungukwa na nchi nane, baadhi zikiwa hazina mwambao wa bahari, jambo linalotupa fursa kubwa ya kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda huu.

Kwa rasilimali hizo, hakuna sababu ya Tanzania kubaki nyuma kimaendeleo. Changamoto kubwa ni namna tunavyoweka vipaumbele na kuzitumia fursa hizo kwa manufaa ya wananchi.

Kwa muda mrefu tumekuwa tukijikita zaidi katika siasa kuliko maeneo ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya muda mrefu, hususan elimu, ujuzi na ubunifu.

Mfano unaojitokeza sasa ni mjadala kuhusu Katiba mpya. Ni muhimu kuwa na Katiba inayokidhi mahitaji ya wakati na inayosaidia kujenga mfumo bora wa kisiasa na utawala. Hata hivyo, Katiba mpya pekee haiwezi kuwa suluhisho la changamoto zote zinazolikabili taifa.

Katiba mpya inaweza kusaidia kutatua baadhi ya changamoto za kisiasa na kiutawala, lakini maendeleo ya kweli yanahitaji zaidi ya Katiba. Yanahitaji watu wenye elimu, ujuzi, uwezo wa kubuni na kutumia teknolojia kuzalisha bidhaa na huduma zenye ushindani.

Tukitazama historia yetu tangu uhuru katika miaka ya 1960, tunaona namna nguvu kubwa ilivyowekezwa katika kujenga misingi ya kisiasa na kijamii, ikiwamo siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Wakati huo, mataifa mengine yaliyopata uhuru karibu na kipindi hicho yalielekeza nguvu kubwa katika elimu, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu.

Leo, baada ya zaidi ya miaka 60 ya uhuru, baadhi ya mataifa hayo yamepiga hatua kubwa katika teknolojia, uzalishaji na uchumi wa maarifa. Hapa ndipo tunapaswa kujiuliza: Je, tunataka kutumia muda mwingi zaidi kujadili siasa pekee au kujenga kizazi kitakachoweza kubadili rasilimali tulizonazo kuwa utajiri?

Katika mjadala huu, nimejikuta nikimkumbuka aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, ambaye Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema. Wakati akiwa madarakani, nilimkosoa aliposema Katiba haikuwa miongoni mwa vipaumbele vyake na mchakato wa Katiba mpya ukawekwa pembeni.

Lakini kadiri ninavyotafakari changamoto za maendeleo, ninaanza kuelewa mtazamo huo. Si kwa maana kwamba Katiba si muhimu, bali kwa kutambua kwamba maendeleo ya taifa hayawezi kusubiri Katiba mpya.

Kuna wanaoamini kwamba Tanzania ikipata Katiba mpya, basi matatizo yake ya maendeleo yatakwisha. Huo ni mtazamo unaoweza kutupotosha katika kuweka vipaumbele. Katiba inaweza kusaidia kutatua changamoto za kisiasa na kiutawala, lakini mkombozi wa kudumu wa maendeleo ni uwekezaji katika watu.

Hapa ndipo elimu, ujuzi na ubunifu vinapokuwa muhimu.

Nikiwa jijini Tanga katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, nimeona fursa kubwa iliyopo nchini. Maadhimisho hayo yanayoendeshwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yameanza Agosti 15 na yataendelea hadi Agosti 24, 2026, katika viwanja vya michezo vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alisema maadhimisho hayo yamewakutanisha wadau kutoka wizara mbalimbali, taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vya ufundi na ufundi stadi.

Kauli mbiu ya mwaka huu, “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” inaelekeza fikra katika eneo ambalo Tanzania inapaswa kulipa uzito mkubwa.

Ofisa Uhusiano Mkuu wa Veta, Sitta Peter alisema maadhimisho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kuona bunifu na teknolojia zilizobuniwa na vijana wa Kitanzania, zikiwamo ambazo tayari zimeingia sokoni kwa kuwezeshwa na Serikali.

Maadhimisho hayo pia yanahusisha Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (Makisatu), mashindano ya ujuzi kwa wanafunzi wa vyuo vya ufundi, makongamano na mijadala ya kimkakati, kliniki ya hakimiliki pamoja na utoaji wa tuzo kwa watafiti waliofanikiwa kuchapisha tafiti zao katika majarida ya kimataifa.

Ofisa Habari wa Nactevet, Dora Tesha alisema mashindano ya ujuzi ya ngazi ya kanda yametumika kama mchujo wa kupata washiriki wa Mashindano ya Ujuzi Kitaifa yanayofanyika Tanga. Kila fani imetoa washindi watano bora waliofuzu kushiriki mashindano hayo.

Washindi watapata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya ujuzi ya Afrika na baadaye ya kimataifa. Haya ni mashindano ya kwanza kufanyika nchini tangu Tanzania ipate uanachama wa WorldSkills Africa.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk Batilda Burian alisema ameguswa na bunifu alizoziona, akieleza kuwa zina umuhimu katika kuhamasisha vijana kujifunza ujuzi kupitia elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

Huo ndio mwelekeo tunaopaswa kuupa nguvu.

Tanzania haiwezi kujenga uchumi imara kwa kutegemea rasilimali pekee. Rasilimali bila maarifa zinaweza kubaki ardhini, lakini maarifa yanaweza kubadili rasilimali kuwa thamani, ajira na utajiri.

Kinachofanyika Tanga kinapaswa kuwa sehemu ya mtazamo mpana wa kitaifa.

Tunahitaji kuongeza uwekezaji katika elimu bora, ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko, sayansi, teknolojia na ubunifu.

Author

admin

Follow Me
Other Articles
Previous

KONA YA MALOTO: Huyu ndiye Brian Mundubile, Tundu Lissu wa Zambia

Next

NIKWAMBIE MAMA: Mkulima na mfugaji ni gego na ufizi, havitengani

Recent Posts

  • Serikali yaeleza kusuasua mradi wa Hospitali ya Singida – 3
  • FYATU MFYATUZI: Naunda tume tatu kuchunguza tume
  • Upinzani na safari ya ujenzi wa kizazi kipya chenye ushawishi
  • NIKWAMBIE MAMA: Mkulima na mfugaji ni gego na ufizi, havitengani
  • UCHAMBUZI WA MAYALA: Elimu, ujuzi, ubunifu ndiyo msingi wa maendeleo

Recent Comments

  1. A WordPress Commenter on Hello world!

Archives

  • August 2026

Categories

  • Habari
  • Magazeti
  • Michezo
Copyright 2026 — Habarimpya. All rights reserved. Blogsy WordPress Theme