Skip to content
-
Subscribe to our newsletter & never miss our best posts. Subscribe Now!
Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

  • Home
  • Sample Page
  • Home
  • Sample Page
Close

Search

  • https://www.facebook.com/
  • https://twitter.com/
  • https://t.me/
  • https://www.instagram.com/
  • https://youtube.com/
Subscribe
Michezo

KONA YA MALOTO: Huyu ndiye Brian Mundubile, Tundu Lissu wa Zambia

By admin
August 19, 2026 4 Min Read
Comments Off on KONA YA MALOTO: Huyu ndiye Brian Mundubile, Tundu Lissu wa Zambia

Rais Hakainde Hichilema ataendelea kuiongoza Zambia kwa muhula wa pili. Halikuwa daraja rahisi kuvuka. Mpinzani wake mkuu, Brian Mundubile, amempa ushindani wenye nguvu. Hata hivyo, wastani wa matokeo ambayo wamepata, yanaweza yasionekane yakiakisi ushindani uliokuwapo.



Rais Hichilema amepata kura 2,965,326, ambazo ni asilimia 61 ya waliojitokeza kupiga kura, ambao namba yao ni 5,028,616. Mundibile kura zake ni 1,856,217, asilimia 38. Wagombea wengine 11, hakuna hata mmoja aliyeweza kupata japo asilimia moja ya kura. Dhahiri, ulikuwa uchaguzi wa wawili.

Katika muhula wake wa kwanza, Hichilema aliweza kufanya mageuzi chanya ya kiuchumi. Pamoja na hivyo, Mundubile aliweza kujenga ushawishi kwa umma kwamba ukuaji wa uchumi Zambia hauendani na hali ngumu ya maisha ya wananchi. Ni hoja hii ya ugumu wa maisha na malalamiko kuhusu haki za binadamu, zilizomfanya Mundubile ampe changamoto pevu Hichilema.

Uchaguzi Mkuu wa Zambia 2026, ulikuwa wa saba kwa Hichilema kugombea. Ameshinda mara mbili. Ya kwanza ilikuwa Uchaguzi Mkuu 2021, alipomshinda Rais aliyekuwa madarakani, Edgar Lungu. Kabla ya hapo, Hichilema aligombea urais Uchaguzi Mkuu 2016, alipotoka wa pili nyuma ya Lungu, kwa tofauti ndogo, asilimia 50.4 dhidi ya 47.6. Mwaka 2015, Hichilema alikabiliana na Lungu, kuwania urais ili kumalizia muhula, kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Michael Sata.

Mwaka 2011, Hichilema alikuwa kwenye makaratasi ya kupigia kura za urais Zambia, alipotoka wa tatu nyuma ya Sata, na Rais wa zamani wa nchi hiyo, Rupiah Banda. Mwaka 2008, Hichilema alikuwa wa tatu, nyuma ya Banda, aliyeshinda, na Sata aliyetoka wa pili. Mwaka 2006, ndiyo ilikuwa mara ya kwanza Hichilema kutokeza kuwania urais, na aliangukia namba tatu, aliyeshinda alikuwa Levy Mwanawasa, Sata alikuwa wa pili.

Maana yake ni kuwa Hichilema alikuwa kwenye mnyukano ambao anaujua vema. Akiwa na umri wa miaka 64 sasa, mara yake ya kwanza kuwania urais alikuwa na miaka 44. Alichomoza katikati ya vigogo wa siasa wa nchi hiyo, Rais Mwanawasa na Rais Sata. Akakabiliana mara tatu na Rais Lungu, ya tatu akamwondoa madarakani. Upande wa Mundubile, umekuwa uchaguzi wake wa kwanza.

Zambia, nchi tajiri wa madini ya shaba, imekuwa katikati ya ushindani wa China na Marekani, zinazoshindania uwekezaji wa madini hayo. Uchaguzi wake uliofanyika Agosti 13, 2026, ulikumbwa na misukosuko na machafuko. Usiku wa uchaguzi, watu 11 walikamatwa, wakiwamo viongozi wa upinzani. Ukamatamaji huo ulihusisha kurushiana risasi, Mundubile akiwa eneo la tukio.

Baada ya ghasia hizo, siku iliyofuata, Tume ya Uchaguzi Zambia (ECZ), iliahirisha kuhesabu kura, kufuatia ripoti kwamba maofisa wa uchaguzi walifanyiwa vurugu, vilevile karatasi za kupigia kura ziliibwa. Mundubile alisema, alikuwa na taarifa ya uwezekano wa matokeo kubadilishwa ili kumpa ushindi Hichilema. Upande wa Hichilema, walijibu kuwa Mundubile alikuwa akiongopa.

Mundubile pia alisema kuwa mamlaka za Zambia zilikuwa zinatumia mbinu za Tanzania, na akasema “Zambia siyo Tanzania.” Kauli hiyo, iliweza kumpambanua Mundubile kama mwanasiasa anayeweza kutamka maneno makali bila kuzingatia athari za kidiplomasia. Mathalan, angetangazwa mshindi, bila shaka angehitaji muda wa kutibu kauli yake, kabla ya kupata uhuru wa kufanya kazi na Tanzania.

Mapema kabisa, Mundubile aliahidi kuyagomea matokeo, na alisema angefungua kesi dhidi ya ECZ. Hata hivyo, mchambuzi wa siasa Zambia, Greg Musiker, wa kampuni ya ushauri wa mambo ya siasa na usalama, inayoitwa Signal Risk, akizungumza na Shirika la Habari la Reuters, alisema ni vigumu kwa kesi ya Mundubile kufanikiwa.

Kuanzia aina yake ya siasa, matamshi na matokeo, Mundubile anapita kwenye njia za Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu. Uchaguzi Mkuu Tanzania 2020, Lissu alikimbilia ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania kuomba hifadhi, kisha akakimbia nchi chini ya ulinzi wa ubalozi. Mundubile, alikimbilia kwenye shirika moja la Umoja wa Taifa, akiwa na aliyekuwa mgombea mwenza wake, Makebi Zulu. Taarifa zinasema tayari Mundubile na Zulu wameshatoroka Zambia

Lissu yupo mahabusu akikabiliwa na kesi ya uhaini. Mundubile anatafutwa na mamlaka za Zambia ili aunganishwe kwenye kesi ya uhaini, yeye akiwa mshitakiwa namba moja. Mundubile anatuhumiwa kuongoza genge la kijeshi, lenye silaha, lililokuwa na malengo ya kuipindua serikali. Bila shaka, asili ya kesi hiyo ni mapigano ya bunduki, baina polisi Zambia na timu ya Mundubile, usiku wa uchaguzi.

Brian Muntayalwa Mundubile ni mwanasheria, kama Lissu. Mundubile ana elimu pia ya uhasibu. Alizaliwa Januari 5, 1971, kwenye mji wa Mporokoso, Kaskazini ya Zambia. Mundubile alichomoza kisiasa kupitia chama cha Patriotic Front (PF), akagombea na kushinda ubunge jimbo la Mporokoso, mwaka 2016. Chini ya uongozi wa Rais Lungu, Mundubile alitumikia nafasi mbalimbali kwenye baraza la mawaziri, ikiwamo kuwa Mnadhimu wa Serikali.

Kuanguka kwa PF kwenye uchaguzi wa mwaka 2021, hivyo United Party for National Development (UPND) cha Hichilema kuongoza serikali, Mundubile alichaguliwa kuwa Kiongozi wa Upinzani kwenye Bunge la Zambia. Nafasi hiyo aliitumikia kuanzia mwaka 2021, ulipofika mwaka 2023, Mundibile alikoma kuwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni kutokana na mabadiliko ndani ya PF.

Mundubile alichomoza na kukua kisiasa akiwa mfuasi wa Lungu. Juni 2025, Lungu alifariki dunia. Baada ya hapo Mundubile aliweza kuibuka kama nyota wa mchezo wa upinzani, hivyo kushawishi muungano wa vyama vya upinzani Zambia, Tonse Alliance, kumteua kuwa mgombea urais Januari 2026. Chama chake, PF, hakikubaliana na ushirikiano na Tonse, hivyo kumtenga kuelekea Uchaguzi Mkuu Zambia 2026.

Ukiacha gharama za maisha, demokrasia na haki za binadamu, Mundubile aliendesha kampeni zake akijipambanua kama mwarobaini wa umaskini wa Wazambia, kilimo, na ukosefu wa ajira. Huyo ndiye Mundubile, ambaye kwa msamiati wa wanasoka, alimlaza Hichilema na viatu, yaani alimpa mechi ngumu kwelikweli. Huyo ndiye Mundubile, Tundu Lissu wa Zambia.

Author

admin

Follow Me
Other Articles
Previous

Pilikapilika Stendi ya Magufuli, Latra yatoa kibali kwa shuttle

Next

UCHAMBUZI WA MAYALA: Elimu, ujuzi, ubunifu ndiyo msingi wa maendeleo

Recent Posts

  • NIKWAMBIE MAMA: Mkulima na mfugaji ni gego na ufizi, havitengani
  • UCHAMBUZI WA MAYALA: Elimu, ujuzi, ubunifu ndiyo msingi wa maendeleo
  • KONA YA MALOTO: Huyu ndiye Brian Mundubile, Tundu Lissu wa Zambia
  • Pilikapilika Stendi ya Magufuli, Latra yatoa kibali kwa shuttle
  • MAGAZETINI LEO JUMATANO AGOSTI 19/2026,MAJI CF YAWAINUA WAJASIRIAMALI WENGI WAANZISHA WATEJA WAKIMBILIA..

Recent Comments

  1. A WordPress Commenter on Hello world!

Archives

  • August 2026

Categories

  • Habari
  • Magazeti
  • Michezo
Copyright 2026 — Habarimpya. All rights reserved. Blogsy WordPress Theme