Pilikapilika Stendi ya Magufuli, Latra yatoa kibali kwa shuttle
Dar es Salaam. Baada ya wamiliki wa mabasi kutii amri ya Serikali, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imewataka kutumia magari madogo ya shuttle kusafirisha abiria kutoka Stendi ya Magufuli iliyopo Mbezi Luis kwenda maeneo mengine, huku mabasi makubwa yakitakiwa kuanzia na kumalizia safari zake katika kituo hicho.
Hatua hiyo imekuja wakati wa utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alilolitoa Agosti 11, 2026, likiwataka wamiliki wa mabasi kurejesha shughuli za kupakia na kushusha abiria katika Stendi ya Magufuli ndani ya siku saba.
Ofisa Mfawidhi wa Latra katika Stendi ya Magufuli, Rukia Kibwana, amesema kampuni zinazohitaji kuwafikisha abiria wao katikati ya jiji au maeneo mengine zinapaswa kutumia shuttle, badala ya mabasi makubwa kuondoka na abiria kutoka stendi kwenda kwenye ofisi zao.
“Tunataka mabasi yote yapakie na kushusha abiria katika Stendi ya Magufuli. Kampuni inayohitaji kuwafikisha abiria katikati ya jiji itumie shuttle,” amesema Rukia.
Basi la kampuni ya Abood likiwa limesimama katika kituo chake kilichopo eneo la Shekilango, karibu na Ubungo Plaza, eneo hilo aghalabu hujaa mabasi mengi yakiwa yamejipanga ya kampuni hiyo, hasa nyakati za asubuhi na jioni kupakia abiria kwenda mikoa tofauti.
Amesema hakuna kampuni itakayoruhusiwa kuchukua abiria katika ofisi zake na kuwapeleka Stendi ya Magufuli kwa kutumia basi kubwa, akieleza kuwa watakaokiuka utaratibu huo watachukuliwa hatua.
Kwa mabasi yanayotumia Barabara ya Bagamoyo, amesema yanatakiwa kuanzia safari Stendi ya Magufuli na kutumia Barabara ya Goba kuelekea Tegeta.
Hatua hiyo imeanza kubadili sura ya maeneo ya Shekilango hadi Magomeni, ambayo kwa muda mrefu yalikuwa na msongamano wa mabasi yaliyokuwa yakipakia na kushusha abiria kwenda mikoa mbalimbali.
Mabasi 200 yarejea Magufuli
Rukia amesema utekelezaji wa agizo hilo umeanza kuonesha mafanikio baada ya zaidi ya mabasi 200 kurekodiwa katika mfumo wa Stendi ya Magufuli ndani ya saa 24, kutoka wastani wa mabasi 150 yaliyokuwa yakiingia na kutoka kwa siku.
Amesema mafanikio hayo yametokana na elimu iliyotolewa kwa kampuni za mabasi kwa ushirikiano na ofisi ya mkuu wa wilaya, ambapo maofisa walikwenda katika maeneo yenye ofisi nyingi za mabasi, ikiwamo Shekilango.
“Kuanzia saa tisa mchana wengi walianza kuleta magari yao na hadi sasa ni zaidi ya magari 200 tumeshayarekodi kwenye mfumo wetu,” amesema.
Mabasi yakataliwa kuondoka na abiria
Katika utekelezaji wa agizo hilo, Mwananchi ilishuhudia baadhi ya mabasi yaliyotaka kuondoka na abiria Stendi ya Magufuli kwenda kwenye ofisi zao mjini na maeneo mengine yakizuiwa na kuamriwa kuwashusha.
Basi moja lililotoka nje ya nchi lilionekana likisimamishwa katika geti la kutokea Stendi ya Magufuli, huku askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani wakikagua mabasi yaliyokuwa yakitoka mikoani kuhakikisha hayaondoki na abiria nje ya utaratibu.
Mkurugenzi wa Habari kwa Umma wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo, amesema kampuni wanachama zimetekeleza uamuzi huo, huku wakiendelea kutafuta nafasi ya kukutana na mkuu wa mkoa kwa ajili ya kuzungumzia changamoto zilizojitokeza.
“Tangu Agosti 13 hadi sasa tunafanya jitihada za kumtafuta mkuu wa mkoa ili tuzungumze naye. Barua tulishatuma. Naamini tukishafanya mazungumzo naye tutatoa msimamo wetu,” amesema Mwalongo.
Meneja Stendi ya Magufuli
Kaimu Meneja wa Stendi ya Mabasi cha Magufuli, Naamini Leonard, amesema stendi hiyo imepangwa kuhudumia mabasi takribani 500 kwa siku.
Hata hivyo, amesema baada ya baadhi ya kampuni kuanzisha vituo vyao nje ya stendi hiyo, idadi ya mabasi yaliyokuwa yakiingia na kutoka kituoni ilishuka hadi kufikia takribani mabasi 150 kwa siku.
Leonard amesema stendi hiyo ina uwezo wa kuegesha na kuhudumia mabasi 200 kwa wakati mmoja katika eneo lake la ndani.
Hata hivyo, uwezo huo hauzuii kuhudumia mabasi 500 kwa siku kwa kuwa huduma zinaendeshwa kwa saa 24, na kila basi hupewa muda wa takribani saa mbili kupakia abiria na kuondoka, hivyo kuwezesha mabasi mengine kuingia na kutumia nafasi hiyo.
Leonard amesema uongozi wa stendi umejipanga kuboresha huduma za kijamii, ikiwamo vyoo, maeneo ya kukaa abiria na udhibiti wa wapiga debe, huku huduma za usafiri zikitarajiwa kuendelea kwa saa 24.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amesema kila anayejihusisha na biashara ya usafirishaji katika wilaya hiyo atalazimika kuanza safari katika Stendi ya Magufuli.
Amesema basi litakalokiuka utaratibu huo halitaruhusiwa kutumia Barabara ya Shekilango kuelekea Mwenge wala Barabara ya Mlimani City kuelekea Mwenge.
“Njia pekee utakayoweza kutumia ni Barabara ya Goba kama unaelekea Bagamoyo, au njia ya Chalinze kama unaelekea Kibaha,” amesema.
Msando amesema utekelezaji huo si kuwaonea wafanyabiashara, bali ni kuhakikisha shughuli za usafirishaji zinafanyika kwa utaratibu, usalama na uwajibikaji.
Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa licha ya baadhi ya watu kujaribu kulizuia.
Mizigo yawekewa utaratibu
Kuhusu usafirishaji wa mizigo, Msando amesema Serikali haijazuia huduma hiyo, bali imeweka utaratibu ambao wasafirishaji wanapaswa kuufuata.
Amesema kumekuwa na mizigo inayosafirishwa bila kufuata utaratibu, hali ambayo baadhi ya kampuni zimekuwa zikitumia kama mwanya wa kupakia abiria baadaye.
“Hatuzuii usafirishaji wa mizigo, tunachosisitiza ni kufuata utaratibu mzuri,” amesema.
Amesema Serikali haiwezi kuruhusu kampuni kutumia kisingizio cha kusafirisha mizigo, wakati huo huo zikikusanya abiria katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Abiria walalamikia gharama
Pamoja na Serikali kusisitiza kuwa utaratibu huo unalenga kuboresha huduma, baadhi ya abiria wameeleza kuwa unawaongezea gharama za usafiri kutoka Stendi ya Magufuli hadi kufika maeneo wanakokwenda.
Yudas Joachim, mkazi wa Manzese, amesema awali mabasi aliyokuwa akitumia kutoka Morogoro yalikuwa yakimfikisha karibu na nyumbani, lakini sasa atalazimika kutumia takribani Sh5,000 zaidi kwa usafiri na mizigo kutoka stendi hadi nyumbani.
Ameiomba Serikali kuangalia namna ya kupunguza gharama hizo ili utaratibu huo usiwe mzigo kwa wananchi.
Mariam Ngoma, mkazi wa Mbagala, amesema hana tatizo na mabasi kuanzia na kumalizia safari Stendi ya Magufuli, lakini ameshauri Serikali kuangalia gharama za usafiri wa umma.
Pia, ameiomba Serikali kuboresha barabara zinazotumiwa na wasafiri kuelekea Mbagala kutokana na foleni zinazoweza kuongeza muda wa safari.
Kicheko kwa wafanyabiashara
Kwa upande wa wafanyabiashara katika Stendi ya Magufuli, kurejea kwa mabasi kumewapa matumaini baada ya biashara zao kudorora kutokana na magari mengi kupakia abiria nje ya kituo hicho.
Said Rajabu, amesema awali mabasi yalipokuwa yakipakia abiria katika ofisi zao mjini, yalipofika stendi yalikuwa yakichukua abiria wachache, wakati mwingine wasiozidi watano.
Amesema hali hiyo iliathiri biashara, lakini kurejea kwa mabasi kumeanza kuleta ahueni.
Aisha Bakari, mjasiriamali katika stendi hiyo, amesema awali alikuwa akipata takribani Sh30,000 kwa siku licha ya kuamka saa 10 usiku.
Amesema baada ya mabasi kuanza kurejea, mapato yake yameongezeka na kufikia Sh60,000 kwa siku na anaamini yataongezeka kadiri siku zinavyoendelea.
Shekilango yapata sura mpya
Katika ziara ya Mwananchi eneo la Shekilango leo, Agosti 18, 2026, ilishuhudiwa mabadiliko ya mandhari baada ya mabasi kuanza kuondoka katika maeneo yaliyokuwa yakitumika kama vituo vya kupakia na kushusha abiria.
Msongamano wa mabasi umepungua, lakini shughuli za ukataji tiketi na upokeaji wa mizigo bado zinaendelea katika ofisi za kampuni hizo.
Ofisi za mabasi yakiwamo Katarama, BM, Happy Nation na Abood zinaendelea na ukatishaji tiketi, huku mawakala wakiendelea kutafuta abiria.
Mizigo ya wasafiri pia imeonekana ikiwa imepangwa nje ya baadhi ya ofisi hizo na kuandikwa majina ya wahusika.

