Shechambo Chris
August 31, 2026
72 views
0 Comments

Iran imefanya mashambulizi kwenye kambi mbili za kijeshi za Marekani nchini Jordan, kwa kutumia makombora ya ndege zisizo na rubani (drones), ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Iran, mashambulizi hayo yalilenga kambi za kijeshi za Marekani za King Hussein na Al-Azraq nchini Jordan.
Hatua hiyo imekuja baada ya Marekani kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya kijeshi ya Iran katika kisiwa cha Larak, kusini mwa Iran.
Tehran imesema mashambulizi yake dhidi ya vituo vya Marekani yalikuwa jibu la moja kwa moja kwa operesheni hiyo ya Marekani.
Kwa upande wa Jordan, jeshi la nchi hiyo limesema mifumo yake ya ulinzi wa anga ilinasa makombora yaliyoelekezwa katika maeneo yake, mamlaka za Jordan zimeripoti kuwa hakuna vifo wala majeruhi vilivyothibitishwa kutokana na mashambulizi hayo.
Marekani imekuwa na uwepo wa kijeshi nchini Jordan, ambayo ni mshirika muhimu wa Washington katika Mashariki ya kati,kwa sababu hiyo mashambulizi hayo yameongeza wasiwasi kuhusu uwezekano wa mvutano kati ya Marekani na Iran kuenea zaidi katika eneo hilo.
Marekani imesema mashambulizi yake dhidi ya Larak yalilenga kuzuia vitisho kwa usafiri wa meli katika eneo la Strait of Hormuz, njia muhimu kwa usafirishaji wa mafuta duniani.
Iran, kwa upande wake, imekosoa vikali hatua hiyo ya Marekani na kuahidi kujibu mashambulizi yoyote dhidi ya maeneo yake.
Na Tereza Muga
