Global Publishers
August 29, 2026
66 views
0 Comments

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amempa pole Deogratius John Ndejembi baada ya kuapishwa rasmi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais Samia amesema Ndejembi sasa amebeba jukumu kubwa la kuwatumikia Watanzania, akitoa kauli hiyo leo Jumamosi, Agosti 29, 2026, katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, muda mfupi baada ya hafla ya kuapishwa kwake.
Ndejembi ameapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, George Mcheche Masaju, na kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Makamu wa Rais kabla ya kutangaza kujiuzulu.

Uteuzi wa Ndejembi ulipata ridhaa ya Bunge jana Ijumaa, Agosti 28, 2026, baada ya jina lake kuwasilishwa na Rais Samia kwa ajili ya kuthibitishwa kuwa Makamu wa Rais.
Bunge lilimthibitisha Ndejembi kwa asilimia 100, hatua iliyofungua njia kwa ajili ya kuapishwa kwake na kuanza rasmi majukumu ya Makamu wa Rais.
Akizungumza baada ya kiapo hicho, Rais Samia amemtakia Ndejembi mafanikio katika kutekeleza majukumu yake mapya, huku akimueleza kuwa nafasi hiyo ni dhamana kubwa kwa taifa.



