Dar es Salaam. Maumivu ya tumbo, kujaa gesi, kiungulia na kichefuchefu ni miongoni mwa dalili zinazowasumbua watu wengi, lakini kwa baadhi yao tatizo hilo limekuwa likijirudia hata baada ya kutumia dawa walizopewa hospitalini.
Vimelea vya bakteria aina ya H. Pylori ni miongoni mwa homa za matumbo zinazosumbua wengi, ambazo husababisha michubuko kwenye ukuta wa tumbo na kusababisha vidonda vya tumbo.
Madaktari wanasema moja ya sababu zinazoweza kuchangia hali hiyo ni maambukizi ya bakteria aina ya Helicobacter pylori (H. pylori), huku wakibainisha changamoto inayojitokeza ya bakteria huyo kutokuitikia baadhi ya dawa zinazotumika katika matibabu.
H. pylori ni bakteria anayeweza kuishi kwenye mfumo wa chakula na kusababisha uvimbe wa ukuta wa tumbo na vidonda vya tumbo. Maambukizi ya muda mrefu ya bakteria huyo bila kutibiwa yanaweza pia kuongeza hatari ya saratani ya tumbo.
Ugonjwa huo si mgeni nchini Tanzania, na kwa mujibu wa wataalamu, maambukizi yake ni ya kawaida katika sehemu nyingi duniani.
Kwa Jeremiah Isdory, tatizo la maumivu ya tumbo limekuwa likimrudia mara mbili ndani ya kipindi cha miezi sita, licha ya kupata matibabu.
“Nilikuwa na maumivu ya tumbo kwa muda mrefu sana. Mwanzoni nilidhani ni kubadilika kwa ratiba yangu ya kazi kulikonifanya nikae bila kula kwa muda mrefu, lakini nilipoenda hospitali iligundulika nina vidonda vya tumbo na nikapata matibabu. Baada ya miezi miwili tatizo lilijirudia,” amesema.
Mgonjwa mwingine amesema alitibiwa H. Pylori kwa dozi za mwezi mzima zaidi ya mara mbili mpaka alipohama hospitali.
“Nilienda hospitali nyingine, nikapewa dawa za wiki mbili. Hapo zilinisaidia yule mdudu kupotea.”
Alipoulizwa kuhusu changamoto hiyo, Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Hamad Nyembea amesema matibabu ya H. Pylori ni kwa kutumia dawa za antibiotiki kwa kuzingatia mwongozo wa matibabu wa Wizara ya Afya.
“Aidha, kama ilivyo ugonjwa mwingine, amesema baada ya kumaliza dozi mgonjwa anapaswa kupima ili kujiridhisha kama amepona, na endapo bado ana vimelea hupaswa kuendelea na matibabu kwa mujibu wa muongozo. Hivyo, kuna nyakati ambapo mgonjwa anatakiwa kutumia dawa zaidi,” amesema Nyembea.
Amesisitiza kuwa wizara inaendelea kusimamia matumizi ya miongozo ya matibabu.
Kwa mujibu wa mwongozo wa dawa, tiba ya awali ya H. Pylori inahusisha mchanganyiko wa dawa tatu ambazo ni PPI, Clarithromycin na Amoxicillin. Usugu wadawa unaweza kufanya dawa hizi za mstari wa kwanza zisifanye kazi, hivyo mgonjwa huhamishiwa katika dawa za mstari wa pili.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Agosti 19, 2026 Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini wa Hospitali ya Aga Khan, Dk Masolwa Ng’wanasai, amesema H. pylori ni bakteria anayehitaji matibabu maalumu na wagonjwa hawapaswi kuanza kutumia dawa kabla ya kufanyiwa uchunguzi na kupewa maelekezo na daktari.
Kwa mujibu wa daktari huyo, changamoto kubwa inayoshuhudiwa kwa sasa ni baadhi ya dawa kutofanya kazi kwa ufanisi kama ilivyotarajiwa, hali inayoweza kuhusishwa na usugu wa bakteria dhidi ya dawa.
“Kwa uzoefu wetu, siku za hivi karibuni imetokea changamoto ya usugu wa dawa za mdudu huyu. Baadhi ya dawa ambazo zimekuwa zikitumika kwa muda mrefu, kwa sasa hazitibu vizuri,” amesema.
Amesema katika baadhi ya mazingira mgonjwa anaweza kuhitaji kupewa dawa nyingine au rufaa endapo dawa zinazohitajika hazipatikani katika kituo anachotibiwa.
Hata hivyo, Dk Ng’wanasai amesema hadi sasa hawajapata utafiti wa kitaifa unaoonyesha ukubwa wa tatizo la usugu wa H. pylori nchini Tanzania.
“Mpaka sasa bado hatujaona utafiti wowote ambao umefanyika hapa nchini kuhusu changamoto hii,” amesema.
Daktari Ngwegwe Damas wa Hospitali ya Wilaya ya Serengeti amesisitiza umuhimu wa wananchi kuacha kujinunulia dawa kwenye famasi bila kufanyiwa uchunguzi.
Amesema hatua hiyo inaweza kufanya mgonjwa kutumia dawa isiyofaa, kutumia dozi isiyo sahihi au kuchangia kuibuka kwa usugu wa dawa.
“Ni muhimu sana watu kuzingatia matibabu sahihi ya hospitali bila kujitibu wenyewe au kwenda duka la dawa kupewa dawa bila kufanya vipimo. Hii itasaidia mgonjwa kupata matibabu sahihi kulingana na ukubwa wa tatizo,” amesema.
Dk Damas pia ameshauri mgonjwa aliyepatiwa matibabu ya H. pylori kufanyiwa kipimo tena baada ya muda unaofaa uliopendekezwa na daktari, badala ya kuhitimisha kwamba amepona kwa sababu tu dalili zimepungua.
“Ni muhimu sana kupima tena baada ya wiki nne za matibabu ili kuthibitisha kwamba bakteria ameondoka kikamilifu na kuondoa changamoto ya ugonjwa kujirudia,” amesema.
Kwa ujumla, Daktari Bingwa Mshauri wa Magonjwa ya Figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Dk Kessy Shija, amesema matumizi yasiyo sahihi au ya muda mrefu ya baadhi ya dawa yanaweza kuchangia usugu wa vimelea.
“Wakati mwingine kuna dawa zinaweza kuwa zimetengeneza usugu. Mgonjwa anapokuja kila mara kuna usugu unaotokea,” alisema.
Amesema hali hiyo inaweza kumfanya mgonjwa aendelee kuwa na dalili hata baada ya kutumia dawa, hivyo si kila mgonjwa anayelalamika maumivu baada ya matibabu anapaswa kupewa dawa zilezile bila uchunguzi zaidi.
Dk Shija pia amesema wagonjwa wanaopata tatizo linalojirudia wanapaswa kutoa historia yao yote ya matibabu kwa daktari.
“Mgonjwa anatakiwa kujieleza vizuri kwa daktari kwamba nilishatibiwa kwa dawa aina hii na hii au nilishapima mara kadhaa na kupewa dawa hii, ili sasa daktari aone njia sahihi ya kuweza kumsaidia,” amesema.
Kwa mujibu wa daktari huyo, kubadilisha madaktari mara kwa mara bila mgonjwa kueleza historia yake ya matibabu pia kunaweza kufanya historia ya ugonjwa isipate picha kamili na hivyo kuchelewesha kupata tiba inayofaa.
Wataalamu wamesema H. pylori inaweza kuenea kati ya watu, hasa katika mazingira yenye usafi duni na upatikanaji mdogo wa maji salama.
Njia zinazoweza kuchangia maambukizi ni pamoja na matumizi ya maji au chakula kilichochafuliwa na bakteria, pamoja na kutonawa mikono vizuri baada ya kutoka chooni na kabla ya kuandaa au kula chakula.


