Brighton Yaichakaza Aston Villa 4-0, Liverpool Yaokolewa Na Penalti Ya Dakika Za Mwisho

Brighton imeanza kwa kishindo msimu wa 2026/27 wa Ligi Kuu England baada ya kuichapa Aston Villa mabao 4-0 katika mchezo uliochezwa Jumapili, Agosti 23, 2026, kwenye Uwanja wa Amex.

Brighton ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya nane baada ya Victor Lindelöf kujifunga mwenyewe.

Dakika 10 baadaye, Maxim De Cuyper aliongeza bao la pili na kuifanya Brighton kuendelea kutawala mchezo.

Jack Hinshelwood aliendelea kuiumiza Aston Villa baada ya kufunga mabao mawili ndani ya dakika mbili, akitikisa nyavu dakika ya 30 na 31 na kuifanya Brighton kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 4-0.

Hali ilizidi kuwa ngumu kwa Aston Villa dakika ya 40 baada ya João Gomes kuonyeshwa kadi nyekundu kufuatia kumchezea vibaya mchezaji wa Brighton.

Villa hivyo ilimaliza kipindi cha kwanza ikiwa pungufu kwa mchezaji mmoja, huku Brighton ikiwa tayari imeweka msingi wa ushindi mkubwa.

LIVERPOOL YAOKOLEWA DAKIKA ZA MWISHO

Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu England, Liverpool imelazimishwa sare ya mabao 2-2 na Newcastle United kwenye Uwanja wa St James’ Park.

Newcastle ilianza kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya tano kupitia Anthony Elanga.

Liverpool ilirejea kipindi cha pili na kusawazisha kupitia Cody Gakpo dakika ya 55, kabla ya Joe Willock kuirudisha Newcastle kifua mbele dakika mbili baadaye.

Liverpool iliendelea kusaka bao la kusawazisha hadi dakika za mwisho, ambapo ilipata penalti katika muda wa nyongeza.

Dominik Szoboszlai alitulia na kufunga mkwaju huo dakika ya 90+9, akiipa Liverpool pointi moja katika mchezo wake wa kwanza wa msimu.

Matokeo hayo yameifanya Liverpool kuanza kampeni ya msimu wa 2026/27 kwa sare, huku kocha mpya Andoni Iraola akianza rasmi safari yake katika Ligi Kuu England.

Stori na Haika Urio | GPL – TUDACO