Skip to content
-
Subscribe to our newsletter & never miss our best posts. Subscribe Now!
Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

  • Home
  • Sample Page
  • Home
  • Sample Page
Close

Search

  • https://www.facebook.com/
  • https://twitter.com/
  • https://t.me/
  • https://www.instagram.com/
  • https://youtube.com/
Subscribe
Habari

Upinzani na safari ya ujenzi wa kizazi kipya chenye ushawishi

By admin
August 19, 2026 7 Min Read
Comments Off on Upinzani na safari ya ujenzi wa kizazi kipya chenye ushawishi

Dar es Salaam. Kwa zaidi ya miongo mitatu tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, upinzani nchini Tanzania umejengwa na viongozi wenye haiba waliogeuka kuwa alama katika vyama vyao.



Umaarufu wa viongozi hao uliviimarisha vyama husika na viongozi hao walipovihama vyama hivyo, umaarufu wake ulipotea na kuviinua vyama walivyohamia, jambo linaloonyesha namna nguvu ya wanasiasa zinavyovibeba vyama.

Freeman Mbowe alibeba sura ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba akakibeba Chama cha Wananchi (CUF), Augustino Mrema akawa sura ya TLP, James Mbatia akaiendeleza NCCR-Mageuzi huku Maalim Seif Sharif Hamad akiwa nguzo ya CUF upande wa Zanzibar na baadaye ACT-Wazalendo.

Vipo pia vyama vilivyowahi kusikika enzi za viongozi fulani na baadaye kufifia katika majukwaa ya kisiasa baada ya viongozi wake wa awali kuondoka kwenye ulingo wa siasa.

Baadhi ya vyama hivyo ni Democratic party (DP) chini ya uongozi wa Mchungaji Christopher Mtikila. Hata hivyo, leo wengi wanasema DP kimepoteza nguvu hiyo tangu mwanasiasa huyo aliyejizolea umaarufu kutokana na msimamo wake mkali na sanaa yake ya uwasilishaji wa hoja jukwaani iliyowavutia wengi, alipofariki dunia.

Mchungaji Mtikila alifariki dunia mwaka 2015 kwa ajali ya gari akiwa katika harakati za uchaguzi mkuu wa mwaka huo, hata hivyo licha ya DP kupata uongozi mpya na kuendelea kushiriki uchaguzi mkuu, jina lake limefifia.

Kwa muda mrefu, nguvu za vyama hivyo zilionekana kutegemea zaidi viongozi hao kuliko taasisi zenyewe. Lakini leo wote hao wameondoka, hawapo tena katika nafasi walizokuwa wakishikilia.

Leo, vigogo hao katika siasa za upinzani za Tanzania hawapo tena. Mjadala unaojitokeza miongoni mwa wadau ni kama kuondoka kwao kumedhoofisha upinzani au kumefungua ukurasa mpya wa siasa za upinzani Tanzania.

Wachambuzi wa siasa wanasema mwisho wa enzi za vigogo waliodumu miongo kadhaa katika uongozi wa vyama vya upinzani hakujazima siasa za upinzani Tanzania, badala yake, vyama vinapitia mageuzi yanayochochewa na viongozi wapya, mazingira ya kisiasa na matarajio ya wananchi.

Kila chama na hatua tofauti

Wachambuzi wanasema kuwa mabadiliko ya uongozi yamekuwa na matokeo tofauti na kila chama kimekuwa na mapito tofauti huku baadhi ya vyama vikionyesha mafanikio kutokana na mabadiliko hayo na vingine vikipotea kwenye ramani kutokana na migogoro iliyodumu baada ya mageuzi ya uongozi.

Mwandishi na mchambuzi wa siasa, Absalom Kibanda, anasema si sahihi kuweka vyama vyote katika kapu moja kwa sababu kila chama kimepitia mazingira tofauti.

Kwa mtazamo wake, ACT-Wazalendo ndiyo mfano wa chama kilichofanikiwa kupita kipindi kigumu cha mpito baada ya kumpoteza Maalim Seif Sharif Hamad.

“Licha ya Maalim Seif kuwa nembo ya siasa za upinzani Zanzibar kwa miongo mingi, kuondoka kwake hakujakisambaratisha chama. Badala yake, ACT-Wazalendo kimeendelea kuonyesha utulivu wa kiuongozi na kuendelea kushiriki siasa bila migogoro mikubwa ya ndani,” anasema.

Anafafanua kuwa hali hiyo inaonesha kuwa chama kimejenga taasisi zinazoweza kuendelea hata baada ya kuondoka kwa kiongozi mwenye ushawishi mkubwa.

Chadema na siasa za mapambano

Kwa zaidi ya miaka 20, Freeman Mbowe alikiongoza Chadema na kukijenga kutoka chama kidogo hadi kuwa chama kikuu cha upinzani nchini. Uongozi wake ulihusishwa zaidi na siasa za majadiliano, kujenga mtandao wa chama na kuimarisha miundombinu ya kisiasa.

Miaka 21, iliyoanza mwaka 2004 ilikoma mwaka 2025, ikipokelewa na Tundu Lissu, kiongozi anayebeba ajenda mpya. Lakini safari ya kuelekea kizazi kipya haikuwa rahisi.

Kibanda anakumbusha kuwa mabadiliko hayo yalianza kwa tofauti za kimtazamo kati ya Mbowe na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu. Baadaye tofauti hizo zilihamia kwenye ushindani wa uenyekiti ambapo Lissu aliibuka mshindi na Mbowe akaondoka madarakani.

“Hata hivyo, tangu wakati huo, chama kimeendelea kupitia kipindi cha mvutano wa ndani huku wakati huohuo kikijaribu kujijenga upya chini ya uongozi mpya,” anasema.

Kibanda anaona si sahihi kusema Chadema imepoteza mwelekeo. Badala yake, anasema chama kimepata nguvu mpya kupitia mazingira yanayowakabili viongozi wake.

Kuwekwa kizuizini kwa mwenyekiti mpya na kesi zinazowakabili baadhi ya viongozi wake kumeongeza hamasa kwa wafuasi na kukifanya chama kutumia mazingira hayo kama sehemu ya kujenga ujumbe wake wa kisiasa.

Kwa maoni yake, kama uchaguzi ungefanyika katika mazingira yenye uhuru mpana wa kisiasa, Chadema bado kingekuwa na uwezo wa kushinda idadi kubwa ya nafasi za uongozi.

Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Chifu Mwaihojo Mwasapile anasema tofauti kati ya Mbowe na Tundu Lissu si udhaifu bali ni mabadiliko ya mtindo wa uongozi.

Anasema Mbowe alikuwa kiongozi wa mazungumzo, mwenye uwezo wa kujenga makubaliano na kuendesha siasa za utulivu huku kwa upande mwingine akimtaja Lissu kuwa amekuja na siasa za ushindani mkali, msimamo usioyumba na mapambano ya wazi dhidi ya mfumo anaouona hauwatendei haki wapinzani.

Mwasapile anatumia mfano wa soka kuelezea tofauti hizo akisema: “Mbowe alikuwa kama mchezaji anayepiga mpira wa kulemba lakini kwa ufanisi mkubwa, wakati Lissu ni mchezaji wa nguvu anayeshambulia kwa kasi lakini bila rafu,” anasema.

Kwa mtazamo wake, katika mazingira ya sasa ya kisiasa, mshambuliaji mwenye nguvu anaweza kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuvutia wananchi kuliko kiongozi anayesisitiza zaidi mazungumzo.

Tofauti na ACT-Wazalendo na Chadema, CUF kimeonekana kuwa na matokeo tofauti kufuatia mabadiliko ya uongozi. Wachambuzi wanasema chama hicho kimepoteza ushawishi wake.

Kwa mujibu wa Mwasapile, Profesa Ibrahim Lipumba licha ya kuendelea kubaki ndani ya chama lakini kuondoka kwake katika nafasi ya juu ya uongozi kuliacha pengo kubwa ambalo halijazibwa kikamilifu.

Anasema kwa miaka mingi Lipumba alikuwa zaidi ya mwenyekiti, alikuwa nguzo iliyokifanya chama kitambulike kitaifa.

Kutokuwapo kwa nguvu hiyo ya kisiasa kumepunguza mvuto wa CUF na kufanya chama hicho kupoteza sehemu kubwa ya ushawishi wake wa zamani.

Katika mtazamo huo, mchambuzi wa siasa na utawala, Profesa Mohamed Makame anasema mabadiliko katika uongozi wa vyama vya siasa hayaepukiki na kwamba lazima viongozi wajenge utamaduni wa kukubali mabadiliko hayo.

Kwa mujibu wake, kila mabadiliko lazima yatakuwa na matokeo yake, akifafanua kuwa vyama vya siasa vitaendelea kubadilika kadiri jamii nayo inavyobadilika, hivyo jamii inapaswa kukubaliana na mabadiliko hayo.

Katika mtazamo huo, NCCR-Mageuzi, kilichowahi kutikisa siasa za Tanzania, hasa katika uchaguzi wa mwaka 1995, kinatajwa kuwa miongoni mwa vyama vinavyopoteza uelekeo wake kutokana na athari za mabadiliko ya uongozi.

Hata hivyo, Kibanda anasema chama hicho kilianza kuyumba baada ya kuondoka kwa Mrema, akifafanua kuwa tangu hapo hadi sasa ni vigumu kukiweka NCCR-Mageuzi katika kundi la vyama vyenye nguvu ya kisiasa nchini.

Hali hiyo inaonyesha namna ambavyo chama kilishindwa kujenga taasisi imara zinazoweza kuendelea bila kutegemea umaarufu wa mtu mmoja.

Kwa mujibu wa Mwasapile, mazingira ya sasa ya kisiasa yamebadilisha kabisa msingi wa nguvu za upinzani. Anasema hapo awali, vyama vilitegemea haiba ya viongozi waliovibeba, lakini leo nguvu hiyo imehamia kwa wananchi wenyewe.

Kwa maoni yake, matukio yanayogusa jamii, yakiwamo kesi zinazowahusu baadhi ya wanasiasa wa upinzani, madai ya utekaji na mazingira mengine yanayoibua mijadala kuhusu haki za kisiasa, yameongeza hamasa ya wananchi kutaka mabadiliko.

Anasema wananchi wengi wanaanza kuamua misimamo yao kutokana na mazingira wanayoishi badala ya kutegemea haiba ya mtu mmoja.

Kwa sababu hiyo, anaamini ni vigumu kupima nguvu ya upinzani kwa kuangalia viongozi pekee bila kuzingatia mazingira mapana ya kisiasa yanayobadilika kila wakati.

Mbali na matukio, mabadiliko ya kizazi nayo yanatajwa kuchochea mtazamo tofauti kuhusu ustawi wa kisiasa nchini.

Kwa mtazamo wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, kizazi kipya maarufu kama Gen Z, hakikubaliani na mifumo ya zamani ya maisha.

Anasema ni kizazi kinachotaka mabadiliko, uwajibikaji wa watumishi na watendaji wa umma, haki za kisiasa na mifumo huru ya uchaguzi hali inayochangia kukua na kuimarika kwa upinzani nchini.

Dk Bagonza anasema; “Kizazi hiki hakiogopi wala hakirudishwi nyuma na vitisho wala matumizi ya nguvu ya mamlaka za serikali, badala yake kinataka kuwa huru kufikiri na kusikilizwa kinapotoa maoni yake yanayodai mabadiliko na ushiriki wa jamii katika ulinzi wa rasilimali, uongozi na uamuzi unaogusa jamii.”

Kwa mtazamo huo, kizazi kipya cha viongozi wa upinzani kinaingia katika mazingira tofauti kabisa na yale yaliyowakuta waanzilishi wa vyama hivyo kwa kuwa kizazi cha kwanza kilikuwa na jukumu la kujenga vyama na kuvitambulisha kwa wananchi tofauti na kizazi cha sasa kinachokabidhiwa jukumu la kuvijenga kuwa taasisi zinazoweza kuishi bila kutegemea mtu mmoja.

Pamoja na mazingira hayo, historia ya vyama vya upinzani Tanzania inaonyesha kuwa viongozi wenye haiba walikuwa msingi muhimu wa ukuaji wake katika awamu za mwanzo za mfumo wa vyama vingi.

Vyama vingi vilisimama na kupata ushawishi mkubwa katika jamii kutokana na majina na haiba za watu waliokuwa wakiviongoza au kushiriki kugombea nafasi za uongozi.

Baadhi ya vyama vilivyopata umaarufu miaka ya nyuma, majina ya viongozi ndiyo yaliamua nguvu ya vyama na kuondoka kwao au kuhama na kujiunga vyama vipya kulidhoofisha vyama vya awali kuvipa nguvu mpya vyama hivyo.

Hata hivyo, mabadiliko ya sasa yanaonyesha kuwa siasa zimeanza kubadilika. Ingawa haiba ya viongozi bado ina nafasi, ushawishi wa vyama unaendelea kuathiriwa zaidi na uwezo wake wa kujenga taasisi imara, kusoma mazingira ya kisiasa na kujibu matarajio ya wananchi.

Wachambuzi wanatolea mfano Chadema kilivyogawanyika kufuatia tofauti za mitazamo baada ya mabadiliko ya uongozi ya mwaka 2025 ambayo yalipelekea baadhi ya makada wake kukihama na kujiunga Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Absalom Kibanda mwandishi wa habari anayechambua masuala ya siasa,  anasema licha ya mgawanyiko huo, Chadema kimeendelea kujiimarisha na kujenga hamasa yenye ujasiri mkubwa, tofauti na ambavyo kingeweza kuathiriwa na mgawanyiko huo uliowatoa baadhi ya waliokuwa viongozi waandamizi wa chama hicho.

Kwa mtazamo wa Kibanda,  katika mazingira ya sasa anasema hatima ya upinzani haitategemea nani amechukua nafasi ya uongozi akimrithi nani aliyekuwa na jina gani ndani ya siasa, bali uwezo wa kizazi kipya kujenga vyama vinavyoishi na kushindana kwa nguvu hata pale ambapo viongozi waliobeba utambulisho wa vyama hivyo wanakuwa hawapo tena.

Author

admin

Follow Me
Other Articles
Previous

NIKWAMBIE MAMA: Mkulima na mfugaji ni gego na ufizi, havitengani

Next

FYATU MFYATUZI: Naunda tume tatu kuchunguza tume

Recent Posts

  • Usaliti wa ACT – Wazalendo, Chadema katika sura pana
  • Serikali yaeleza kusuasua mradi wa Hospitali ya Singida – 3
  • FYATU MFYATUZI: Naunda tume tatu kuchunguza tume
  • Upinzani na safari ya ujenzi wa kizazi kipya chenye ushawishi
  • NIKWAMBIE MAMA: Mkulima na mfugaji ni gego na ufizi, havitengani

Recent Comments

  1. A WordPress Commenter on Hello world!

Archives

  • August 2026

Categories

  • Habari
  • Magazeti
  • Michezo
Copyright 2026 — Habarimpya. All rights reserved. Blogsy WordPress Theme