Agizo la Chalamila Stendi ya Magufuli lapingwa
Dar es Salaam. Abiria wameendelea kupinga uamuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, wa kutaka mabasi ya mikoani kuanzia na kumalizia safari katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, wakitaka suala hilo litazamwe upya kwa kuzingatia masilahi ya abiria, hususan wanaoishi mbali na Mbezi Luis.
Uamuzi huo umeibua kumbukumbu ya agizo kama hilo lililowahi kutolewa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, ambalo pia lilikumbana na malalamiko kutoka kwa wananchi na hatimaye kubadilishwa.
Makalla, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, alitoa agizo hilo Julai 2021, akitaka mabasi yanayoingia na kutoka Dar es Salaam kutumia Kituo cha Mabasi cha Magufuli kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria. Agizo hilo lilitolewa wakati akisikiliza kero za wafanyabiashara katika kituo hicho, ambao walilalamikia baadhi ya mabasi kupakia na kushusha abiria nje ya kituo, hivyo kupunguza wateja katika eneo hilo.
Hata hivyo, agizo hilo lilikutana na upinzani kutoka kwa wananchi waliodai kuwa kulazimisha abiria wote kufika Mbezi Luis kungeongeza gharama na usumbufu, hasa kwa wanaotoka au kuelekea maeneo ya kusini na katikati ya jiji.
Malalamiko hayo yalihusu pia abiria waliokuwa wakishushwa Magufuli baada ya safari ndefu, kisha kulazimika kutafuta usafiri mwingine kwenda maeneo yao ya makazi ilihali baadhi ya mabasi yanayowashusha yanaelekea wanakokwenda.
Hoja hiyo ilifikia Serikali Kuu, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi kwa wakati huo, Innocent Bashungwa, Agosti 30, 2022, alimtaka Makalla kukutana na wadau na wamiliki wa mabasi, ili kuweka utaratibu shirikishi usiowaongezea wananchi adha.
Bashungwa alisema wakati huo kuwa baadhi ya abiria wanaoingia Dar es Salaam kupitia Magufuli walihitaji mabasi hayo kuendelea hadi vituo vya mabasi vilivyojengwa na sekta binafsi mjini ili kuwafikisha karibu na maeneo yao.
Alisisitiza kuwa lengo la Serikali la kutumia Kituo cha Magufuli linaweza kutekelezwa bila kuwaongezea wananchi gharama za kutafuta usafiri mwingine baada ya kushushwa Mbezi Luis.
Baadaye, Makalla aliruhusu vituo binafsi vilivyohakikiwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kuendelea kutoa huduma, kwa sharti la mabasi kuingia na kutoka Kituo cha Magufuli.
Chalamila alitoa agizo hilo Agosti 11, 2026, akizitaka kampuni za mabasi zinazotoa huduma nje ya Kituo cha Mabasi cha Magufuli kuhamia kituoni hapo na kuanza kutoa huduma zake kutoka eneo hilo.
Mkuu huyo wa Mkoa alitoa muda wa siku sita kwa kampuni hizo kutekeleza agizo hilo, akisisitiza kuwa ifikapo leo, Agosti 17, 2026, mabasi yote ya masafa marefu yanapaswa kuwa yameondoka katika vituo vingine na kurejea Kituo cha Magufuli.
Gazeti hili lilifika katika maeneo yenye ofisi za kampuni mbalimbali za mabasi, ikiwamo Ubungo, Shekilango, Manzese, Argentina na Magomeni, na kubaini kuwa shughuli za usafirishaji wa abiria bado zinaendelea kama kawaida.
Baadhi ya abiria waliozungumza na gazeti hili walipinga agizo hilo, akiwamo Leonard Munisi aliyesema viongozi wanapotoa maamuzi wanapaswa kuzingatia mabadiliko ya maisha na mahitaji ya abiria, akisema miundombinu ya usafiri iliyopo inapaswa kutumika kwa manufaa ya abiria.
“Kama suala ni mapato ya Kituo cha Magufuli, Serikali inaweza kuangalia namna ya kuongeza tozo kidogo kwa mabasi yanayopakia au kushusha abiria nje ya kituo hicho. Serikali isiangalie tu mapato, iangalie pia ubinadamu na namna ya kuwasogezea wananchi huduma karibu,” amesema.
Naye William Makali amesema agizo hilo linaweza kuwaongezea abiria usumbufu, ikiwamo kuvutwa mabegi na wapiga debe, kutapeliwa na hata kuibiwa wanapofika Magufuli kutafuta usafiri.
“Sisi tunaishauri Serikali iangalie changamoto zilizopo na kufanya uamuzi kwa masilahi mapana ya abiria ili vituo vilivyo nje ya Magufuli viendelee kufanya kazi kwa kuwa vina faida nyingi kuliko hasara,” amesema.
Kwa upande wake, Elly Mumbungu, mkazi wa Mbagala, amesema agizo hilo litawaumiza wananchi wa kipato cha kawaida, akisema mabasi yanayowafikisha maeneo ya Mbagala, Mbande, Kigamboni na Chanika yamekuwa yakirahisisha maisha yao.
“Sasa ukiniambia nishuke Mbezi, gharama ya kutoka huko hadi nyumbani nani atabeba? Maisha ni magumu,” amesema.
Baadhi ya wamiliki na wadau wa usafirishaji wa mabasi nchini wameitaka Serikali kulitazama kwa jicho la ziada agizo hilo, wakisema utekelezaji wake unaweza kuwaongezea changamoto abiria.
Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo, amesema baada ya Kamati Tendaji kukutana, wamekubaliana kuwasiliana na viongozi wa Serikali ili kujadiliana kuhusu agizo hilo.
“Hadi sasa bado tunaendelea kufanya jitihada za kwenda kuzungumza nao, na barua tayari zilishatumwa. Kwa hiyo, bado hatuna msimamo tulioufikia kuhusu jambo hilo zaidi ya kwenda kukubaliana kuongea na viongozi,” amesema.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi ya Tilisho, John Tilisho, amesema Serikali inapaswa kuwapa kipaumbele wamiliki ambao wamewekeza katika kujenga vituo na ofisi zao, ili wananchi wapate huduma karibu na maeneo wanayoishi.
Amesema kauli ya Chalamila, si mbaya, lakini ingekuwa vyema viongozi kutembelea vituo mbalimbali na kujionea changamoto zilizopo.
“Kwenda Mbezi ni jambo zuri, lakini kwa watu wanaosafiri kwenda mikoa ya Kaskazini itakuwa changamoto kwa sababu ya njia,” amesema.
Tilisho amesema barabara ya Goba ambayo baadhi ya mabasi yatapaswa kutumia ina changamoto kutokana na kuwa nyembamba na ina matuta mengi, hali ambayo inaweza kuongeza muda wa safari.
“Ukisema unatoka Stendi ya Magufuli kufika Moshi muda fulani, hicho kitu hakipo. Changamoto itakuwa kubwa,” amesema.
Amesema Serikali inaweza kushirikiana na wamiliki wa vituo binafsi kwa kuwawekea utaratibu wa kulipa tozo au ada zinazostahili badala ya kuwalazimisha kuhamia Magufuli.
Kwa upande wake, mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya Esther Luxury, Joseph Ngelleuya, amesema hawapingani na Serikali na watafuata maelekezo yatakayotolewa, akisema mwisho wa siku anayebeba athari za uamuzi huo ni abiria.
“Tukishapewa maelekezo ni kuyafuata. Hatuwezi kupingana na Serikali. Tunawasikiliza na kutenda wanalolitaka, kwa sababu katika suala hili mwathirika ni mwananchi,” amesema.
Mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya Shabiby, Ahmed Shabiby, amesema agizo la kuondoa vituo visivyo rasmi katikati ya Jiji linapaswa kuungwa mkono, lakini amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na masilahi ya abiria.
Amesema Latra inaruhusu mtu mwenye sifa na kituo kilichokidhi vigezo kuendesha shughuli hizo, hivyo vituo vilivyoidhinishwa vinapaswa kuruhusiwa kufanya kazi.
“Watu wakipata kituo ambacho kimekubaliwa na Latra waachwe waegeshe,” amesema.
Hata hivyo, Shabiby amesema mabasi yote yanapaswa kupitia Kituo cha Magufuli ili kukaguliwa na Serikali kukusanya mapato.
Ametoa mfano wa Dodoma, ambako mabasi huanzia katika vituo vyao, lakini hulazimika kupitia stendi kuu kwa ajili ya ukaguzi na malipo ya ushuru.
Amesema utaratibu huo unaweza kuleta usawa kwa Serikali kupata mapato huku abiria wakiruhusiwa kuanzia safari zao katika vituo vilivyo karibu nao.
Naye msemaji wa Kampuni ya Kimbinyiko, Hamisi Maneno, ameunga mkono agizo la Chalamila, akisema uegeshaji wa mabasi katika maeneo yasiyo rasmi umeongeza msongamano na kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara.
Amesema suluhisho ni kuwa na vituo maalumu, huku akitaka mabasi yote yalazimishwe kupitia stendi kwa ajili ya ukaguzi na ulipaji wa ushuru.
Ametolea mfano eneo la Urafiki, akisema limekuwa likitumika kama eneo la maegesho kwa namna inayosababisha changamoto kwa watumiaji wengine, huku baadhi ya vituo vikikosa huduma muhimu kwa abiria.
Kaimu Meneja wa leseni Latra, Pateli Ngereza, amesema kwa Mkoa wa Dar es Salaam mabasi yote yanayotoka Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Ziwa yanapaswa kuishia kituo cha mabasi kilichopo Mbezi Louis (yaani Magufuli Bus Terminal).
Huku yale mabasi yanayotoka Mikoa ya Kusini yakipaswa kuishia kituo cha mabasi Mbagala kilichopo Wilaya ya Temeke jijini humo.
Imeandikwa na Tuzo Mapunda, Nasra Abdallah, Habel Chidawali (Dodoma) na Janeth Joseph (Kilimanjaro)
