Vijana wa Mwanjelwa walivyogeuza kucha, rangi kuwa dili
Mbeya. Soko la Mwanjelwa lililopo jijini Mbeya ni miongoni mwa masoko yanayowakutanisha wafanyabiashara wa bidhaa na huduma mbalimbali, lakini ndani yake kuna kundi la vijana lililogeuza upakaji rangi na ubandikaji kucha kuwa chanzo cha kipato.
Kwa vijana hao, kazi hiyo imekuwa fursa ya kujitafutia kipato halali na kujikwamua kiuchumi, huku wakikabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwamo vishawishi kutoka kwa baadhi ya wateja na mazingira ya kazi.
Kwa nyakati tofauti, Mwananchi imefika sokoni hapo na kuzungumza na baadhi yao kuhusu kazi hiyo na maisha yao kwa ujumla.
Twabi Mawea, mkazi wa Tunduru mkoani Ruvuma, anasema tangu alipowasili Mbeya miaka miwili iliyopita, kazi hiyo imekuwa mkombozi kwake.
Anasema aliacha masomo ya sekondari kutokana na changamoto za maisha na kuamua kujikita katika shughuli hiyo.
“Kwa siku naingiza takriban Sh50,000, kutegemea aina ya huduma anayohitaji mteja. Kiwango cha chini ni Sh28,000 kwa mtu mmoja. Sijutii kazi hii, imenipa heshima kifamilia,” anasema.
Rafael Jackson, mkazi wa Ikuti anayefanya kazi hiyo kwa mwaka mmoja sasa, anasema imebadilisha maisha yake ikilinganishwa na alipokuwa akiendesha bodaboda.
“Nina uhakika wa mahitaji muhimu ya familia. Kwa siku naweza kuondoka na Sh60,000 baada ya kugawana na bosi wangu, ingawa wakati mwingine kipato huongezeka kulingana na mzunguko,” anasema.
Kijana mwingine, Erick Samuel, anasema kazi hiyo imemwezesha kufungua kituo cha uwakala wa fedha na hana mpango wa kuacha kwa kuwa anaona fursa kubwa ya kujikwamua.
Anasema kazi hiyo haihitaji elimu kubwa na inafanywa na watu wenye viwango tofauti vya elimu.
Hata hivyo, vijana hao wanasema baadhi ya wateja huleta changamoto, hasa wanapohitaji huduma nyumbani.
Mawea anasema wakati mwingine mavazi na mienendo ya baadhi ya wateja huwaweka katika mazingira magumu.
“Tunakutana na vishawishi vingi. Mteja anakuita nyumbani kwake, lakini mazingira unayokutana nayo yanaweza kukupa ugumu. Kwa kuwa tumeamua kutafuta riziki kupitia kazi hii, tunavumilia,” anasema.
Jackson anasema kwa kuwa sehemu kubwa ya wateja wao ni wanawake, baadhi ya mazingira wanayokutana nayo yanahitaji umakini mkubwa.
Vijana hao pia wanasema wanachukua tahadhari dhidi ya maambukizi kwa kutumia barakoa na glovu, hasa wanapokutana na wateja wenye michubuko.
Samuel anasema pia huwa makini na vumbi linalotokana na kucha bandia pamoja na harufu ya rangi wanazotumia.
“Tunashika miili ya watu tofauti na wengine huwa na michubuko. Pia hatujui madhara ya baadhi ya rangi tunazotumia, hivyo tunashauriwa kuvaa barakoa na glovu,” anasema.
Akizungumzia suala la mitaji, Mawea anasema licha ya kipato wanachopata, bado wanakabiliwa na changamoto ya mitaji na hawakuwa na taarifa za kutosha kuhusu mikopo inayotolewa na Serikali kupitia halmashauri.
“Bado hatujawahi kuomba mikopo kwa sababu hatukujua mapema. Sasa tutashirikiana na wenzangu kuomba. Hii ni kazi halali na tunalipa kodi, tatizo ni mtaji tu,” anasema.
Emmy Casian, mteja wa huduma hizo, anasema vijana hao wanafanya kazi muhimu inayosaidia kuwabadilisha wateja mwonekano.
Happy Sanga anasema baadhi ya wateja wanapaswa kuepuka kuingiza masuala binafsi wakati wa kupata huduma kwa kuwa hali hiyo inaweza kuwaathiri wahudumu.
Mbunge wa Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge, anasema atatembelea makundi mbalimbali ya wajasiriamali, likiwamo kundi hilo, kusikiliza changamoto zao na kutafuta namna ya kuboresha mazingira ya biashara.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Mkuu wa Kitengo cha Maliasili, Utalii na Hifadhi ya Mazingira, Anamary Joseph, anasema Serikali imetenga asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya mikopo kwa vijana, wanawake na makundi maalumu.
Anasema kikundi cha watu kuanzia watano kinaweza kukopa hadi Sh150 milioni kwa ajili ya shughuli za kiuchumi, hivyo kuwataka vijana kutumia fursa hiyo.

