BIDHAA ZA CHAKULA ZISIZOKIDHI MATAKWA YA VIWANGO ZATEKETEZWA .
Na Mwandishi Wetu.
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeendelea kuonesha dhamira yake ya kulinda afya za wananchi baada ya kuteketeza tani 39 za bidhaa za chakula ambazo hazikukidhi matakwa ya viwango, zenye thamani ya takribani Shilingi milioni 149.
Zoezi hilo la uteketezaji lililofanyika leo, Agosti 17, 2026, katika eneo la Mbezi Gongoni, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, ni sehemu ya juhudi za TBS katika kuhakikisha bidhaa zinazopatikana sokoni zinakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.
Kwa mujibu wa Meneja wa TBS Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bi. Noor Meghji, bidhaa hizo zilikamatwa kupitia ukaguzi wa mara kwa mara uliofanywa na wakaguzi wa shirika hilo katika kipindi cha Julai hadi Agosti mwaka huu.
Amesema ukaguzi huo umebaini kuwa baadhi ya bidhaa za chakula zinazouzwa katika masoko mbalimbali hazikuzingatia matakwa ya viwango, jambo ambalo linaweza kuhatarisha afya za watumiaji.
Bi. Meghji alieleza kuwa changamoto kubwa iliyobainika ni uwepo wa bidhaa nyingi ambazo hazikuwa na alama ya ubora pamoja na kukosa maelezo sahihi kwenye vifungashio.
Alifafanua kuwa baadhi ya bidhaa hizo hazikuwa na taarifa zilizoandikwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza, kinyume na matakwa ya Sheria ya Viwango nchini inayotaka maelezo ya bidhaa yawe wazi ili kumwezesha mtumiaji kuelewa bidhaa anayotumia na viambata vilivyomo.
“Ni muhimu kwa watumiaji kusoma maelezo yote yaliyopo kwenye vifungashio kabla ya kutumia bidhaa yoyote. Hii itawasaidia kufahamu bidhaa wanazonunua pamoja na kuhakikisha zinakidhi viwango vinavyotakiwa,” alisema Bi. Meghji.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara kuzingatia sheria na kuhakikisha bidhaa wanazoziingiza au kuziuza zinakidhi viwango vilivyowekwa na mamlaka husika.
Hatua ya TBS kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara sokoni imeendelea kupongezwa na wadau mbalimbali kutokana na mchango wake katika kulinda afya za wananchi pamoja na kuimarisha mazingira salama ya biashara.
Kupitia ukaguzi huo, bidhaa ambazo hazikidhi viwango huondolewa sokoni mapema kabla hazijasambazwa kwa watumiaji, jambo ambalo limeendelea kusaidia kupunguza hatari ya matumizi ya bidhaa zisizo salama.
Hatua hiyo inaonesha wazi kuwa TBS, inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kulinda afya ya jamii kwa vitendo kupitia ukaguzi endelevu unaosaidia kuhakikisha bidhaa zinazofika kwa watumiaji zinakuwa salama, zenye ubora na zinazokidhi matakwa ya sheria za nchi.























