DCEA yateketeza ekari 603 za bangi Morogoro
Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeanza operesheni maalumu ya kuharibu mashamba ya bangi mkoani Morogoro, baada ya kubaini wakulima kuhamia maeneo ya mbali ndani na nje ya Hifadhi ya Mikumi.
Katika operesheni maalumu iliyofanyika kwa siku 14 katika vijiji vya Visengele na Lugenge wilayani Mvomero, DCEA imeteketeza ekari 603 za bangi, kukamata magunia 49 ya bangi na watuhumiwa 13 kwa tuhuma za kujihusisha na kilimo cha dawa hizo za kulevya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumatatu Agosti 17, 2026 Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo operesheni hiyo ni mwendelezo wa kampeni maalumu ya kudhibiti dawa za kulevya zinazozalishwa nchini, hususani bangi, huku akieleza kuwa mamlaka imebaini baadhi ya wakulima wamehamia maeneo ambayo hayajawahi kufikiwa na operesheni za awali.
Amesema pamoja na operesheni kufanyika katika maeneo hayo tangu mwaka 2023, bado wananchi wameendelea kulima bangi ndani ya Hifadhi ya Mikumi na maeneo ya nje ya hifadhi.
“Katika operesheni tulizozifanya safari hii tumegundua kwamba wamelima mbali zaidi ya maeneo ambayo operesheni zilishafanyika awali, wakidhani mamlaka itashindwa kufika katika maeneo hayo,” amesema Lyimo.
Lyimo amesema ukubwa wa mashamba yaliyobainika unaonyesha kuwa kilimo cha bangi bado ni changamoto katika baadhi ya maeneo ya Morogoro, hasa ndani ya hifadhi na katika vijiji vinavyozunguka maeneo ya mapori.
“Maeneo haya yako mbali sana na vijiji na makazi ya wananchi, lakini mamlaka itaweka intelijensia ya kutosha ili kuhakikisha kwamba hizi operesheni na hawa wahalifu tutaendelea kuwakamata,” amesema.

