Dar es Salaam. Suala la uhamiaji linatarajiwa kutawala mjadala katika mkutano wa 46 wa kawaida wa wakuu wa nchi na serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaofanyika leo, Agosti 17, 2026, jijini Durban, Afrika Kusini.
Mkutano huo unaowakutanisha viongozi wa nchi 16 wanachama unafanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Durban, chini ya uenyekiti wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.
Ajenda rasmi ya mkutano huo ni pana na inahusisha maendeleo ya kiuchumi, usalama, ushirikiano wa kikanda, usalama wa chakula pamoja na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya SADC.
Hata hivyo, suala la uhamiaji limeibuka kama moja ya changamoto zinazoweza kuhitaji uangalizi wa viongozi, hasa kutokana na kuongezeka kwa mvutano kuhusu wahamiaji nchini Afrika Kusini na athari zake kwa uhusiano kati ya nchi wanachama.
Mjadala huo unakuja wakati Afrika Kusini ikiendelea kukabiliana na malalamiko ya baadhi ya raia wanaodai wahamiaji wanashindania ajira, huduma za jamii na fursa za kiuchumi.
Takwimu rasmi za serikali ya nchi hiyo zinaonyesha takribani watu milioni 2.4, waliozaliwa nje ya nchi wanaishi nchini humo , na utafiti mwingine ulionyesha idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia milioni 3.1.
Wataalamu wanaonya kuwa changamoto ya uhamiaji haiwezi kutatuliwa na Afrika Kusini pekee kwa kuwa inahusishwa kwa kiasi kikubwa na tofauti za kiuchumi, ajira na fursa zilizopo kati ya nchi za SADC.
Mtazamo huo umeungwa mkono na Taasisi ya Institute for Security Studies (ISS), inayosisitiza kuwa uhamiaji unapaswa kushughulikiwa kama suala la kikanda kutokana na utegemeano wa nchi wanachama.
Kwa mtazamo huo, hatua za nchi moja katika kudhibiti wahamiaji zinaweza kuwa na athari kwa majirani zake, hasa kwa kuwa wananchi wa nchi za SADC wamekuwa wakivuka mipaka kutafuta ajira, biashara, usalama na fursa nyingine za kiuchumi.
Kwa mujibu wa Associated Press (AP), Afrika Kusini imetumia karibu dola milioni 18 kugharamia kuwarejesha wahamiaji katika nchi zao, huku zaidi ya watu 80,000 wakirudishwa au kusaidiwa kurejea katika mataifa yao.
Serikali pia imesema imewakamata karibu watu 60,000 waliokuwa nchini humo bila vibali, wakiwamo zaidi ya 16,000 kwa Julai pekee.
Rais Ramaphosa amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kuonya dhidi ya mgongano kati ya ajenda ya ushirikiano wa kikanda na matendo yanayoweza kuwabagua wahamiaji.
Katika hotuba yake ya Agosti 14, alisema Afrika Kusini haiwezi kuzungumzia ushirikiano katika mikutano ya kikanda wakati ikifanya kinyume chake mitaani, akisisitiza umuhimu wa mshikamano uliojengwa katika historia ya ukombozi wa eneo hilo.
Kauli hiyo inaweka shinikizo zaidi kwa mkutano wa Durban, ambao unafanyika wakati suala la uhamiaji likiwa tayari limezua mijadala mikali ndani ya Afrika Kusini na katika baadhi ya nchi jirani.
Imeandaliwa na Salma Hamis kwa msaada wa mitandao.



Leave a Reply