Wateja wa simu, vifaa vya umeme wanavyopigwa Kariakoo

Written by

in

Dar es Salaam. Simu, vifaa vya umeme vinavyowatesa wanunuzi vuta picha unanunua simu kwenye duka, ukipewa boksi, risiti na hata dhamana ya miezi kadhaa, lakini baada ya siku chache kifaa kinaanza kuganda, betri kuisha haraka au kamera kupoteza ubora.

Huo ni uzoefu ambao baadhi ya wanunuzi wa simu na vifaa vya umeme wameueleza, wakisema changamoto hizo zimekuwa zikiwafanya kuwa na wasiwasi kuhusu hali halisi ya bidhaa wanazonunua.

Malalamiko hayo hayahusu simu pekee, bali pia baadhi ya vifaa vya umeme ikiwamo majokofu, televisheni, pasi na majagi, ambavyo baadhi ya wanunuzi wanasema huanza kupata hitilafu muda mfupi baada ya manunuzi.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa katika biashara ya simu na vifaa vya umeme, zipo bidhaa mpya, zilizotumika na nyingine ambazo zimewahi kufanyiwa ukarabati kabla ya kurejea sokoni.

Changamoto kubwa inayojitokeza ni kwamba wakati mwingine mnunuzi haelezwi kwa uwazi historia ya bidhaa anayoinunua, hali inayoweza kusababisha malalamiko pale kifaa kinapopata hitilafu.

Mkazi wa Malamba Mawili, Dar es Salaam, Shida Mbwana, anasema alifika kununua simu ya Samsung akiwa na Sh400,000, wakati simu mpya aliyokuwa akiihitaji ikiuzwa Sh540,000.

Anasema baada ya kueleza kiasi alichokuwa nacho, alionyeshwa simu iliyotumika kutoka Dubai kwa Sh380,000.

“Tulikuwa tunahitaji simu nzuri ya Samsung, lakini tulipofika tukawaambia tuna Sh400,000 tukaonyeshwa nyingine iliyotumika kwa Sh380,000 na tukaambiwa imetoka Dubai,” anasema.

Anasema walipewa dhamana ya miezi mitatu, lakini baada ya wiki moja kamera ilianza kutoa picha zisizo na ubora huku betri ikiisha chaji haraka.

Waliporudi dukani, anasema waliambiwa simu ilifanyiwa majaribio kabla ya kuondoka na huenda waliiangusha nyumbani.

Tatizo kama hilo lilimkuta Khalfan Mussa, mkazi wa Morogoro, anayesema alibadilisha simu na kuongeza fedha, lakini baada ya wiki mbili kifaa kilianza kusimama na hata simu ikiita, hakikubali kupokea.

“Nimejifunza ukinunua simu ni vizuri uwe na mtu anayeyajua maduka vizuri. Nimeshawahi kupewa simu isiyofanya kazi vizuri na niliporudisha nikaambiwa ni makosa yangu,” anasema.

Mfanyabiashara wa simu, Sheila Mjata, anasema biashara ya kubadilishana simu maarufu kama top-up imekuwa ikiwasaidia wananchi kupata vifaa bora kwa gharama wanazoweza kuzimudu.

Anasema mteja hupeleka simu aliyokuwa akitumia, thamani yake hukadiriwa na kisha kuongeza fedha ili kupata nyingine yenye thamani kubwa zaidi.

Kwa mujibu wake, baadhi ya simu zinazopokelewa huwa na maboksi, chaja na vifaa vyake vya awali, huku zenye hitilafu ndogo zikifanyiwa marekebisho kabla ya kuuzwa tena.

Hata hivyo, anasisitiza kuwa mnunuzi anapaswa kufahamishwa kama simu ni mpya au imeshatumika.

“Bei ya simu iliyotumika haiwezi kuwa sawa na mpya. Maelezo sahihi ni muhimu ili kuepusha malalamiko baadaye na kuitana matapeli,” anasema.

Mfanyabiashara mwingine, Hassan Ramadhani, anasema katika duka lao huuza simu mpya na zilizotumika, lakini huzitenganisha ili mteja ajue anachonunua.

“Zilizotumika huwa wazi na tumezipanga tofauti na bei zake ni za chini, zipo hadi za Sh130,000,” anasema.

Hata hivyo, anasema baadhi ya simu hufanya kazi vizuri dukani, lakini baada ya siku kadhaa mteja hurudi akilalamikia programu kutofanya kazi au chaji kuisha haraka.

Hata hivyo kuna wanaosema baadhi ya simu hurudishwa sokoni zikiwa zimetumiwa sana.

“Nilinunua simu hapa sokoni Arusha kweli niliambiwa ni zilizotumika Dubai, ila nilipoinunua nilibaini ilitumika sana na ninahisi ni hizi za top up, mtu anaitumia ikimsumbua anakwenda kuibadili analipa pesa kidogo anapewa nyingine,”anasema Akida Mrosso.

“Siku wanatumia kichaka cha simu used (zilizotumika)kutoka Dubai kuuza hizi wanazozipata kwa wanaotop up, zinakuwa zimetumika sana na ukitumia kidogo inaharibika na haikarabatiki tena,”anasema Sikudhani Juma, mkazi wa Kilosa.

Akizungumzia ukarabati wa simu, fundi wa simu Mtaa wa Aggrey Dar es Salaam, Mansour Pembe, anasema ukarabati ni sehemu ya kawaida ya biashara hiyo, akieleza kuwa hubadilisha skrini, vioo, nyumba za simu, betri na vipuri vingine.

“Baada ya kutengenezwa, baadhi huuzwa tena kwenye maduka au hata na mafundi wenyewe,” anasema.

Kwa mujibu wake, tatizo si bidhaa kufanyiwa ukarabati, bali mnunuzi kutofahamishwa kuwa kifaa alichonunua kimewahi kutumika au kufanyiwa marekebisho.

Mfanyabiashara wa vifaa vya umeme, Abbas Mahamoud, anasema baadhi ya wateja huchagua bidhaa zilizotumika kwa sababu ya bei kuwa nafuu.

“Si kila mtu anaweza kununua bidhaa mpya. Mtu anaweza kuja na Sh250,000 wakati jokofu jipya ni Sh350,000, hapo tunamwonyesha lililotumika linalolingana na fedha zake,” anasema.

Maria Godfrey anasema amewahi kununua friji ndogo iliyoharibika muda mfupi baadaye, jambo lililomfanya kuwa mwangalifu zaidi anaponunua vifaa vilivyotumika.

Mtaalamu wa uchumi, Sophia Mussa, anasema biashara ya bidhaa zilizotumika inaweza kuwasaidia watu wa viwango tofauti vya kipato kupata vifaa wanavyohitaji.

Anasema changamoto inaanza pale bidhaa iliyotumika au iliyofanyiwa ukarabati inapouzwa kama mpya bila kumweleza mnunuzi historia yake.

“Kuuza bidhaa iliyotumika si tatizo ikiwa mteja anaelezwa hali yake kabla ya manunuzi. Tatizo linakuwa pale inapouzwa kama mpya bila taarifa sahihi,” anasema.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema limebaini wimbi la matukio ya utapeli yanayowalenga wananchi kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumanne, Agosti 4, 2026, Kamanda wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro, alisema baadhi ya watuhumiwa hutumia mbinu mbalimbali kuwahadaa wananchi na kujipatia fedha kwa udanganyifu.

Alisema wamekamatwa watuhumiwa wanaohusika na kuvunja nyumba, kuiba na kununua mali za wizi, zikiwemo simu, luninga, pikipiki, laptop na redio.

Kamanda Muliro aliwataka wananchi kutoa taarifa zenye viashiria vya kihalifu ili zifanyiwe kazi.

Haji Adam, fundi simu na mtaalamu wa teknolojia  anasema hakuna kipimo kimoja kinachoweza kuthibitisha kwa uhakika kuwa simu imetumika, lakini mnunuzi anaweza kufanya ukaguzi maeneo kadhaa kabla ya kuinunua.

Anashauri kwanza kukagua afya ya betri, kwa kuwa baadhi ya simu huonyesha uwezo wake uliobaki na historia ya matumizi. Kwa iPhone, taarifa hizo hupatikana kupitia Settings > Battery > Battery Health & Charging. Ikiwa simu inayodaiwa kuwa mpya ina uwezo wa betri uliopungua, anasema mnunuzi anapaswa kuwa makini.

Kwa baadhi ya simu za Android, taarifa za betri hupatikana kwenye sehemu ya Battery, ingawa hatua hutofautiana kulingana na aina na toleo la simu. Mnunuzi anaweza pia kuangalia battery cycle count ikiwa kifaa kinaonyesha taarifa hiyo, kwani idadi kubwa inaweza kuashiria matumizi ya muda mrefu.

Aidha, anashauri kuangalia Battery Usage ili kuona programu zilizotumika na historia ya matumizi. Simu mpya kabisa kwa kawaida haitakuwa na historia ya matumizi ya muda mrefu.

Pia, mnunuzi akague tundu la kuchajia, chaja na kebo kwa kuangalia mikwaruzo, uchafu au alama za kuchakaa zinazoweza kuonyesha matumizi ya muda mrefu.

Mwisho, anashauri kuangalia kama simu ina akaunti, picha, programu, faili au mipangilio iliyowekwa na mtumiaji mwingine. Simu mpya kwa kawaida huanza kwenye hatua ya awali kwa kila program.

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *