Skip to content
-
Subscribe to our newsletter & never miss our best posts. Subscribe Now!
  • https://www.facebook.com/
  • https://twitter.com/
  • https://t.me/
  • https://www.instagram.com/
  • https://youtube.com/
Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

  • Home
  • Sample Page
  • Home
  • Sample Page
Subscribe
Close

Search

Habari

Mahakama kuamua Kesi ya Lissu Ijumaa

By admin
August 17, 2026 5 Min Read
0

Dar es Salaam. Hatima ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, katika kesi ya uhaini inayomkabili imeingia katika hatua muhimu, baada ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam kupanga Ijumaa, Agosti 21, 2026, kutoa uamuzi mdogo wa kubaini kama ana kesi ya kujibu au la.



Uamuzi huo unakuja baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wake jana Jumatatu, Agosti 17, baada ya kuwaita mashahidi 17 kati ya 30 walioorodheshwa.

Lissu, anafikisha siku 495 akiwa kizuizini hadi leo Agosti 17, 2026, alikamatwa Aprili 9, 2025 katika Wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma, kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema.

Kesi hiyo inatokana na shtaka moja la uhaini chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, likihusishwa na maneno aliyodaiwa kuyatamka Aprili 3, 2025 kuhusu kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Leo Agosti 17, 2026 Jamhuri imeeleza haitaita mashahidi   wote 30 waliokuwa kwenye orodha ikifafanua kuwa baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na kuangalia wa mashahidi waliobaki, umeona uliopo unatosheleza. Hivyo uamuzi wa Agosti 21, 2026 utakaoweka mwelekeo wa hatua inayofuata.

Iwapo mahakama itaona Jamhuri imefeli kujenga kesi, Lissu hatalazimika kuingia katika hatua ya kujitetea na anaweza kuachiwa kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama. Lakini iwapo majaji wataona kuna ushahidi unaomtaka ajibu mashtaka, kesi itaingia katika hatua ya utetezi na Lissu atalazimika kujibu ushahidi uliowasilishwa dhidi yake.

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru, James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Safari ya Lissu mahakamani

Katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja akiwa mahabusu, Lissu amekutana na vikwazo kadhaa vya kisheria, huku baadhi ya mapingamizi yake yakikubaliwa na mengine yakitupiliwa mbali.

Miongoni mwa hatua kubwa ilikuwa Septemba 22, 2025, Mahakama Kuu ilipotupilia mbali mapingamizi yake kuhusu uhalali wa hati ya mashtaka.

Mahakama ilisema hati hiyo ilikuwa inakidhi matakwa ya kisheria, huku suala la nia ya kutenda uhaini likielezwa kuwa ni jambo la ushahidi litakaloamuliwa wakati wa usikilizwaji wa kesi.

Oktoba 2025, Lissu aliwasilisha mapingamizi manne kupinga kupokelewa kwa vielelezo vya video na vifaa vya kuhifadhia taarifa vilivyowasilishwa na upande wa Jamhuri.

Baadaye, katika hatua nyingine ya kesi, aliwasilisha mapingamizi matano kuhusu masuala yanayohusiana na shahidi wa siri na kizimba kilichotengenezwa mahakamani kwa ajili ya mashahidi hao.

Februari 11, 2026, Mahakama Kuu ilitupilia mbali mapingamizi manne kati ya matano, lakini ikakubali moja lililohusu kizimba cha shahidi wa siri.

Mahakama iliamuru kifanyiwe marekebisho ili majaji waweze kumuona shahidi wakati akitoa ushahidi.

Kwa maana hiyo, katika hatua hizo mbili zinazojulikana wazi, Lissu aliwasilisha jumla ya mapingamizi tisa, ingawa si yote yalikuwa na mada moja.

Kati ya mapingamizi hayo, mahakama ilikubali mawili huku moja likihusu kielelezo cha video na jingine kuhusu kizimba cha shahidi wa siri, wakati mengine yalitupwa.

Katika hoja zake Lissu ameieleza mahakama hiyo kuwa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki iliweka msingi wa uthibitishaji wa kosa la uhani ili mshtakiwa awe na kesi ya kujibu kupitia kesi za Grey Likungu Mataka na wenzake dhidi ya Jamhuri na  Hatibu Gandhi na wenzake dhidi ya Jamhuri.

Amesema kuwa mahakama hiyo iliweka masharti matatu ambayo ni mshtakiwa awe na utiifu kwa Jamhuri ya Muungano, nia ya kutenda kosa la uhaini, uthibitisho wa nia hiyo kwa maandishi au kwa matendo ya wazi.

Pia, amedai kuwa mahakama hiyo ilisema maneno matupu hayatengenezi kosa la uhaini isipokuwa kama yataendana na kosa la uhaini, hata hivyo msimamo huo unatumika pale ambapo mshtakiwa wa uhaini ni mmoja.

Kuhusu utiifu amesema kuwa halina mjadala kwani ni  raia wa Tanzania.

Ameeleza kuwa kosa linalotajwa katika kifungu anachoshtakiwa ni kuitishia Serikali, Bunge au Mahakama na lazima nia hiyo idhihirishwe kwa kuchapisha maandishi au kwa kuonesha matendo ya wazi ni kosa la uhaini.

Amesema kuwa kwa kurejea hati ya mashtaka maneno aliyoyatamka ya kuzuia uchaguzi si miongoni mwa makosa  kwa mujibu wa kifungu hicho cha  Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2025 au sheria yoyote nchini.

Amesisitiza kuwa katika maneno hayo hakuna mahali alikotamka Serikali, Bunge wala mahakama, rais, waziri mkuu au mkuu wa mkoa lakini mashahidi hawakuthibitisha akisisitiza kuwa uchaguzi husimamiwa na Tume ya Uchaguzi na si Serikali.

Kuhusu kuchapisha au kuonesha  matendo ya wazi, amedai kuwa Jamhuri haikuweza kuthibitisha kuwa ni yeye aliyechapisha maneno hayo kwenye mtandao wa Youtube wa  Jambo TV na   hata hiyo video hawakuiwasilisha mahakamani.

Badala yake amesema kuwa shahidi wa 17 ambaye ndiye alikuwepo katika mkutano wake alieleza kuwa yeye, shahidi huyo na wenzake watano ndio waliorekodi na kuchapisha video hiyo.

“Kwa hiyo kudhihirisha nia ya uhaini kama ilivyowekwa kwenye  kesi ya Grey na Gandhi haupo na hakuna ushahidi wa nia ya kutenda kosa lolote kwa mujibu wa sheria za Tanzania zinazojulikana”, amesema Lissu.

Amesisitiza kuwa ameshtakiwa kwa kosa lisilokuwepo kisheria kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi na kwamba amekaa gerezani kwa siku 496 kwa kitendo ambacho si kosa la uhaini wala kosa kwa mujibu wa sheria yoyote nchini bali kwa mashtaka ya uonevu na ya kijinga.

Hivyo, ameiomba mahakama iamuru alipwe fidia kwa uonevu huo wa kukaa gerezani kwa muda wote huo kwa mujibu wa kifungu cha 367 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Jamhuri katika hoja zake kupitia Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, ameieleza mahakama kuwa kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa wamethibitisha viini vyote vya kosa la uhaini na kwamba kwa mshtakiwa anapaswa kujitetea.

“Sisi Jamhuri tunaona mshtakiwa ana kesi ya kujibu katika mashtaka alivyoshtakiwa nayo chini ya kifungu  cha 39(2) (d) cha Penal code.

Akichambua hati ya mashtaka, Katuga alidai kuwa kiini cha kwanza cha nia ya kutenda kosa mshtakiwa huyo ni kwamba yeye ni raia wa Tanzania,  anawajibu wa kutii sheria kwa mujibu wa katika ya Muungano wa Tanzania, kiini hicho kina thibitisha kuwa mshtakiwa anakiri kuwa yeye ni Mtanzania

Kiini cha pili, cha nia ya uhaini amesema kuwa maneno aliyoyasema  mshtakiwa ya kukinukisha na kuvuruga uchaguzi yalilenga kuchochea umma  kwa nia ya kuitishia Serikali.

Alidai kiini hicho kimedhibitisha na shahidi wa kwanza, wa 16 na wa tatu, ambapo kwa pamoja walisema maneno ya mshtakiwa ya kwamba watavuruga uchaguzi, yalitishia Serikali kwani ndio ina jukumu la kulinda sheria.

Amesisitiza kuwa kuitishia Serikali lazima mpaka iwe imetishika bali hata kuonesha nia hiyo ni kosa la uhaini chini ya kifungu hicho.

“Tunaomba mahakama ione ushahidi ulitolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka, mshtakiwa anao wajibu wa kujitetea, hivyo anatakiwa aletwe mahakamani kwa ajili ya kujitetea,” amesema  Katuga

Kuhusu ombi la mshtakiwa kulipwa fidia, amesema kuwa hoja hiyo hawataijibu kwa sasa mpaka ambapo Mahakama itamkuta na kesi ya kujibu.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote Jaji Ndunguru amesema kwa kuwa mashahidi ni wengi na hoja ni nyingi wanahitaji kupata muda wa kupitia ushahidi na hoja hizo na Mahakama itatoa uamuzi wake Agosti 21, 2026.

Author

admin

Follow Me
Other Articles
Previous

Nishati mbadala yatajwa kuwa suluhu ya uharibifu wa mazingira

Next

Kinachosubiriwa Ijumaa kesi ya Lissu

No Comment! Be the first one.

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recent Posts

  • GLOBAL EDUCATION LINK YAPELEKA WANAFUNZI 198 CHINA NA 189 INDIA
  • 16 mbaroni kwa tuhuma za kuchoma moto shamba, matrekta ya mwekezaji
  • UBORA WA SHULE ZA ST DOMINIC SAVIO ,WAPONGEZWA NA WAZAZI
  • FEASSA 2026 KUFANYIKA MOROGORO, WANAFUNZI 6,800 KUSHIRIKI MASHINDANO
  • Vijana wa Mwanjelwa walivyogeuza kucha, rangi kuwa dili

Recent Comments

  1. A WordPress Commenter on Hello world!

Archives

  • August 2026

Categories

  • Habari
  • Magazeti
Copyright 2026 — Habarimpya. All rights reserved. Blogsy WordPress Theme