Afrika kugeukia teknolojia ya AI kuimarisha usalama wa mitihani
Arusha. Mabaraza ya mitihani barani Afrika yameshauriwa kutumia mifumo ya kidijitali, uchanganuzi wa data na akili unde (AI) kubaini na kudhibiti udanganyifu wa mitihani unaozidi kuwa wa kisasa, ili kuboresha ubora wa elimu na kuzalisha wanafunzi wenye ushindani katika soko la ajira.
Wito huo umetolewa leo Jumatatu, Agosti 17, 2026, katika mkutano wa 42 wa mwaka wa Jumuiya ya Tathmini ya Elimu Afrika (AEAA), unaofanyika Arusha kwa siku nne na kuwakutanisha zaidi ya wajumbe 350 kutoka nchi 28 za Afrika na mabara mengine.
Mkutano huo ulioandaliwa chini ya uenyeji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), umewakutanisha maofisa wa wizara za elimu, mabaraza ya mitihani, wataalamu wa tathmini na wadau wa elimu kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha mifumo ya tathmini barani Afrika kutokana na kasi ya maendeleo ya teknolojia, hususan matumizi ya AI.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Carolyne Nombo amesema njia za jadi za kulinda usalama wa mitihani hazitoshi tena kukabiliana na changamoto zinazotokana na matumizi ya simu janja, mitandao ya kijamii na AI.
Amesema udanganyifu wa mitihani umebadilika kutoka mbinu za kawaida na sasa unaweza kufanyika kupitia vifaa na majukwaa ya kidijitali yanayowezesha taarifa kusambazwa kwa haraka.
“Usalama wa mitihani haupaswi kuishia katika kuzuia mwanafunzi kuingia na nyenzo zisizoruhusiwa kwenye chumba cha mtihani, bali unapaswa kuanzia hatua ya uandaaji wa maswali hadi utoaji wa matokeo,” amesema.
Amesema hatua hizo zinapaswa kujumuisha uandaaji na uchapishaji wa maswali, usafirishaji na uhifadhi wake, uendeshaji wa mitihani, usahihishaji, uchakataji wa taarifa na utoaji wa matokeo.
“Kadiri teknolojia inavyoendelea, udanganyifu katika mitihani nao unazidi kuwa wa kisasa, huku simu janja, mitandao ya kijamii na AI zikitajwa miongoni mwa changamoto zinazohitaji mifumo mipya ya usalama,” amesema.
Hata hivyo, Profesa Nombo amesema teknolojia hizo hazipaswi kuonekana kama tishio pekee, bali zitumike pia kutafuta suluhisho la changamoto hizo.
“Niwahimize mabaraza ya mitihani barani Afrika kuwekeza katika mifumo imara ya usalama wa kidijitali, uchanganuzi wa data na zana zinazotumia AI ambazo zinaweza kusaidia kubaini viashiria vya udanganyifu na dosari katika mchakato wa mitihani,” amesema.
Kwa upande wake, Rais wa AEAA, Dk Eshetu Kebede Gichoro, amesema pamoja na uwekezaji katika mifumo ya kiteknolojia, nchi za Afrika zinapaswa kuweka sera na miongozo ya wazi ya matumizi ya AI katika tathmini ya elimu.
Amesema miongozo hiyo inapaswa kuzingatia maadili, uwazi, usalama wa data, usawa na haki kwa wanafunzi.
Kwa mujibu wa Dk Gichoro, AI inatoa fursa kubwa za kuboresha mifumo ya tathmini, ikiwamo mitihani inayoweza kubadilika kulingana na uwezo wa mwanafunzi, uchanganuzi wa utabiri na uundaji wa njia binafsi za ujifunzaji.
Hata hivyo, amesema teknolojia hiyo pia inazua maswali kuhusu usawa, maadili na umiliki wa data, hasa kwa nchi zinazotumia mifumo ya kiteknolojia inayotengenezwa nje ya Afrika.
Amesema bara hilo linapaswa kujenga mifumo yake ya tathmini inayounganisha teknolojia na mahitaji yake, badala ya kutegemea mifumo ya nje ambayo huenda isiakisi uhalisia wa Afrika.
“Endapo Afrika haitajenga mifumo yake huru ya tathmini inayounganisha teknolojia, tunahatarisha kuwa watumiaji wa mifumo iliyoagizwa kutoka nje ambayo huenda isiakisi uhalisia wala kutumikia matarajio yetu,” amesema.
Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Ally Mohamed amesema mkutano huo unalenga kutafakari namna mifumo ya tathmini inavyoweza kubadilishwa ili kukabiliana na kuongezeka kwa matumizi ya AI na teknolojia duniani.
Amesema pia mkutano huo unatoa fursa kwa wataalamu kutoka nchi mbalimbali kubadilishana tafiti, uzoefu na ubunifu kuhusu matumizi ya teknolojia katika kuboresha tathmini ya elimu.
“Pamoja na usalama wa mitihani, pia utaangazia namna data inayozalishwa kupitia tathmini inavyoweza kutumika katika kuboresha elimu,” amesema.
Ameongeza kuwa mkutano huo utaangazia pia umuhimu wa kuhakikisha matumizi ya teknolojia hayawaachi nyuma wanafunzi kutoka maeneo yenye changamoto za kiuchumi, vijijini na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu.

