Dar es Salaam. Malumbano ya kisiasa nchini Kenya yameendelea kupamba moto kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, baada ya Rais William Ruto kuwatuhumu baadhi ya wapinzani wake kuwa wanatumwa na “sponsor” ambaye hakumtaja, lakini maelezo yake yakionekana kumlenga Rais mstaafu, Uhuru Kenyatta.
Ruto alitoa kauli hiyo Agosti 13, 2026, mjini Eldoret, Uasin Gishu County, alipozungumza na wananchi baada ya kuhudhuria shughuli katika KDF Recruits Training School (RTS), ambako aliongoza sherehe ya kuhitimu kwa kundi la kwanza la mwaka 2025.
Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanazungumzia kijembe hicho kilichotolewa na Ruto kuwa kinachangamsha siasa za Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, ambapo hoja mbalimbali zitatolewa majukwaani, huku mwisho wa siku wananchi wakiwa ndio wataamua.
Katika hotuba yake, Ruto aligusia utendaji wa Serikali ya zamani katika miradi ya nyumba za gharama nafuu (Affordable Housing), bima ya afya kwa wote (Universal Health Coverage) na elimu, akidai kuwa mdhamini huyo wa wapinzani wake alishindwa kutekeleza mambo hayo alipokuwa madarakani.
Ingawa hakumtaja kwa jina, maelezo yake yalionekana kumlenga moja kwa moja mtangulizi wake, Kenyatta, ambaye Ruto aliwahi kuwa mshirika wake wa kisiasa akiwa Naibu Rais, kabla ya wawili hao kutofautiana kisiasa.
Ruto, pia, alidai kuwa mdhamini huyo amekwenda kupanga ‘vibaraka’ wake na kuwatuma kushindana naye kuelekea uchaguzi wa 2027, huku akisema hana wasiwasi na wapinzani hao.
Huku akishangiliwa na wananchi, Ruto alisema: “Kila kiongozi anapimwa na ile kazi amefanya, hakuna mtu atakuja kututapeli hapa ati atwambie, ‘oh, sijui kasongo one term, must go’, ati alafu tumpatie kazi, yaani ufala bana.
“Mimi ninawauliza watu wa Eldoret, si nyinyi ni Wakenya? Si mmewahi kupiga kura? Si nyinyi ni mafundi wa siasa? Si mnajua viongozi wote?
“Nataka niwaulize, mkipima wale watu, yule sponsor wao, yule sponsor wao si alishindwa na maneno ya affordable housing? Si alishindwa na mambo ya Universal Health Coverage? Si alishindwa na maneno ya kusomesha watoto wetu?
“Sasa ameenda kupanga vibaraka wake, ati anatuma hapa watu, ati waje washindane na mimi, hawa watu nitawaosha asubuhi na mapema,” amesema Ruto.
Ameongeza kuwa: “Wale watu mmesikia mipango yao? Mmesikia ajenda yao? Mmesikia sera yao? Mmesikia maono yao? Oh, kumbe mnawajua? Wale majamaa hawana mpango… sera… ajenda… maono… hata akili hawana kabisa.”
Sura mbili za siasa za Kenya
Kauli ya Ruto imeongeza mjadala kuhusu sura inayochukua ushindani wa kisiasa nchini Kenya, hasa wakati wanasiasa wanapoanza kujenga hoja kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Profesa Mohammed Makame, amesema malumbano ya aina hiyo ni sehemu ya ushindani wa kisiasa katika mfumo wa vyama vingi, ambapo pande zinazoshindana hutumia hoja mbalimbali kujenga ushawishi kwa wananchi na kuimarisha nafasi zao kuelekea uchaguzi.
Amesema malumbano hayo yanaweza kuwa na sura mbili; kwanza, yanaweza kutumiwa kuonesha uimara wa chama au kiongozi wa kisiasa na kutafuta uungwaji mkono wa wananchi ili kurejea madarakani.
“Vilevile, yanaweza kujikita katika utekelezaji wa ilani na sera, ambapo kila upande hujaribu kuonesha kwa nini unastahili kupewa ridhaa ya wananchi,” amesema.
Amesema vyama vya upinzani kwa kawaida hujikita katika kuonesha udhaifu wa chama kilichopo madarakani, ikiwamo kukosoa utekelezaji wa ilani na kuunganisha hoja hizo na hali halisi inayowakabili wananchi katika masuala ya kijamii na kiuchumi.
“Kwa upande wa Rais Ruto, bila shaka ana nia ya kuendelea na kugombea, hivyo anapambana na vitu vyote viwili. Kwa wale wanaomuunga mkono, watakuwa wakilinda na kutetea yale aliyoyafanya na mabadiliko aliyoyaleta,” amesema.
Amesema Ruto na wafuasi wake, pia, wanahitaji kulinda uimara wa chama chao na kujenga mtaji wa wanachama ambao ni muhimu katika uchaguzi mkuu, huku upande wa pili ukijikita katika kutafuta madaraka kwa kuonyesha mapungufu ya Serikali iliyopo.
Makame amesema katika mazingira hayo, ukosoaji unaweza kuwa wa aina mbili, ikiwamo ule unaochambua kwa kina ukweli na matokeo ya utekelezaji wa Serikali, na ule wa kisiasa unaolenga kujenga uhalali wa kisiasa wa upinzani kwa kuwaaminisha wananchi kuwa Serikali iliyopo haijafanya vya kutosha.
“Lakini pia kuna kukosoa political, kwa maana ya kutengeneza legitimacy (uhalali) ya upinzani kwamba aliyepo madarakani hakuweza kufanya kitu,” amesema.
Amesema mazingira ya kisiasa Kenya yanaweza kuathiriwa na masuala ya kikanda na siasa za makabila, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa sehemu ya mijadala ya kisiasa nchini humo.
“Kauli zinazotolewa na Ruto zinaweza kutafsiriwa kama sehemu ya mkakati wa kujilinda kisiasa kwa kuonesha mambo ambayo Serikali yake imefanikiwa kufanya katika kipindi alichokuwa madarakani, hasa ikiwa ana mpango wa kuomba ridhaa ya wananchi kwa muhula mwingine.
“Anapomwangalia aliyetoka madarakani, naye anamwangalia mpinzani kama ni mpinzani, kwa hiyo ruling party (chama tawala) inakuwa opposition party (chama cha upinzani),” amesema.
Profesa Makame amesema hali hiyo inafanya hata chama kilicho madarakani kuendelea kumtazama mpinzani kama tishio linalopaswa kuzuiwa kupata nafasi ya kuingia madarakani, akibainisha kuwa kauli kama hizo zinaweza kuendelea kuongezeka kadiri uchaguzi wa 2027 unavyokaribia.



Leave a Reply