Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya CCBRT zimepokea Sh200 milioni zilizotokana na mbio za hisani za CRDB Bank Marathon, fedha zinazolenga kuboresha huduma za afya na kuongeza upatikanaji wa matibabu kwa makundi yenye uhitaji.
Katika hafla ilifanyika jana jijini Dar es Salaam, kila taasisi ilikabidhiwa Sh100 milioni, huku tukio hilo likiambatana na ujumbe wa kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi mara kwa mara na kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.
Mbio hizo zilihusisha washiriki wa kilomita tano, 10, 21 na 42 pamoja na mbio za baiskeli za kilomita 65, zikivutia maelfu ya wananchi kutoka makundi mbalimbali nchini.
Mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, ambaye alisisitiza umuhimu wa kuendeleza shughuli zinazowakutanisha wananchi na kuimarisha afya zao ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Hemed ambaye alimwakilisha waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alisema ukiratibu Watanzania kufanya mazoezi unakuwa umeokoa fedha nyingi kwa sababu wagonjwa wengi wanaibiwa kwa mazoezi.
“Kazi hii ambayo tumeifanya leo (jana) kuhakikisha Watanzania wamefanya mazoezi, tumeokoa fedha nyingi za Watanzania kwa sababu zaidi ya asilimia 40 hawakai ndani, wanatibiwa kisaikolojia tu kuwa wanatakiwa kufanya mazoezi,” alisema.
Alisema uchumi wa Tanzania unategemea taasisi za fedha na CRDB imeonesha kwa vitendo na wanachangia mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Kazi hii ambayo CRDB wameifanya inapaswa kuwa endelevu na inalindwa,” alisema Hemed huku akigusia ushiriki wa watu wengi kwenye mbio hizo ni ishara kwamba nchi ipo salama.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Juma Malik Akil, alisema Serikali itaendelea kuunga mkono mipango inayochangia ustawi wa jamii, akieleza kuwa mbio hizo zimekuwa chachu ya kuhamasisha mshikamano, afya na maendeleo ya wananchi.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi, akiambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Grace Magembe, walishiriki katika mbio hizo na kusisitiza kuwa afya kinga ndiyo msingi wa kupunguza mzigo wa magonjwa nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Abdulmajid Nsekela, alisema CRDB Bank Marathon imeendelea kuwa zaidi ya mashindano ya riadha, bali ni jukwaa linalounganisha michezo na dhamira ya kuleta mabadiliko yenye manufaa kwa jamii.
Alisema kupitia mbio hizo, Benki ya CRDB imeendelea kutekeleza falsafa yake ya kurudisha kwa jamii kwa kusaidia sekta ya afya na makundi yenye uhitaji, huku kila mshiriki akiwa sehemu ya safari ya kubadilisha maisha ya Watanzania.
“Safari ya CRDB Bank Marathon imeendelea kuonyesha kuwa michezo inaweza kuwa daraja la kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Kila mwaka tumeshuhudia ongezeko la ushiriki na mchango mkubwa zaidi kwa sekta ya afya,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB Bank Foundation, Oswald Urassa, alimshukuru mgeni rasmi pamoja na washiriki na wadhamini wote kwa kuendelea kuiunga mkono mbio hiyo.
Alisema bodi itaendelea kusimamia sera na miongozo itakayoiwezesha taasisi hiyo kuongeza ufanisi katika kutekeleza miradi yenye manufaa kwa jamii, hususan sekta ya afya.
Kwa niaba ya wadhamini, Ofisa Mkuu wa Fedha wa Sanlam Allianz Tanzania, Samwel Mika, aliyemwakilisha Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, alisema wanafarijika kuwa sehemu ya safari ya CRDB Bank Marathon kutokana na mchango wake katika kugusa maisha ya wananchi.
Aliahidi kuwa Sanlam Allianz Tanzania itaendelea kushirikiana na CRDB Bank Foundation kuhakikisha mbio hizo zinaendelea kuleta matokeo chanya kupitia miradi ya afya na maendeleo ya jamii.
Mbali na kuchangisha fedha, mbio hizo zimeendelea kuwa jukwaa la kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi, kuzingatia lishe bora na kuchukua hatua za mapema katika kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Wizara ya Afya ilieleza kuwa ushiriki wake katika mbio hizo unaendana na mkakati wa kuimarisha afya kinga na kuongeza ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuboresha huduma za afya nchini.



Leave a Reply